• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
MATHEKA: Wizara, idara za serikali ziige IEBC kutii mahakama

MATHEKA: Wizara, idara za serikali ziige IEBC kutii mahakama

Na BENSON MATHEKA

KUMEKUWA na visa vya maafisa wa wizara, idara na mashirika ya serikali kukiuka maagizo ya Mahakama lakini Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeonyesha kwamba haiko katika tapo hili.

Mahakama Kuu mjini Eldoret ilipoiagiza tume kuendelea na zoezi la usajili wa wapigakura lililopaswa kukamilika Jumanne wiki hii, tume hiyo haikupuuza agizo hilo.

Licha ya kuwa inatekeleza mipango yake kwa kutegemea pesa ilizonazo, tume hiyo inayosimamiwa na Wakili Wafula Chebukati, iliamua kufuata mkondo wa sheria.

Iliagiza zoezi hilo kuendelea huku ikiwasilisha kesi kortini kupinga agizo la kuitaka kuendelea na usajili wa watu hadi Novemba 9 kesi iliyowasilishwa Mahakama Kuu ya Eldoret itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Ikifahamu wazi agizo hilo lingeathiri mipangilio ya utendakazi wake hasa kwa kuvuruga bajeti, IEBC ilichagua kutii mahakama inavyotakiwa kuliko kupuuza na kudharau majaji.

IEBC ilitaja kuwa agizo la Mahakama Kuu ya Eldoret, lilitolewa hata kabla ya tume kujibu madai ya mlalamishi aliyeishtaki akitaka iendelee kusajili wapigakura wapya.

Kwa kufanya hivi, Bw Chebukati na tume yake walionyesha kuwa wanaheshimu utawala wa sheria ambao maafisa wakuu wa wizara, idara na mashirika ya serikali wamekuwa wakikaidi.

Inaweza kusemwa kwamba hatua ya IEBC inatokana na ushauri wa mawakili wake na tajiriba ya mwenyekiti wake ambaye ni mwanasheria.

Ikiwa hili ni kweli, inaweza kusemwa pia kuwa maafisa wa serikali wanaokaidi maagizo ya Mahakama huwa wanafanya hivyo makusudi na kudharau sheria za nchi.

Inaweza pia kusemwa kuwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo inafaa kushauri serikali kuhusu masuala ya sheria imetelekeza majukumu yake, inapotosha au kuongoza kwa kudharau mahakama na utawala wa sheria kwa jumula.

Mkondo wa sheria umeweka mwongozo wa kufuata kwa yeyote asiyeridhika na uamuzi wa Mahakama jinsi IEBC ilivyofanya kwa kukata rufaa chini ya ombi la dharura.

Mkondo wa sheria sio kukosoa uamuzi kwenye mikutano ya hadhara na kuchochea umma dhidi ya Mahakama jinsi baadhi ya maafisa wa serikali wamekuwa wakifanya.

Utawala wa sheria ndio nguzo ya demokrasia halisi na unafaa kuheshimiwa jinsi IEBC ilivyofanya.

Maafisa wa serikali wakizingatia utawala wa sheria, kila raia atafanya hivyo.

Wakuu wa wizara, idara na mashirika ya serikali waige makamishna wa IEBC kwa kuheshimu maagizo ya Mahakama ili kuhakikisha utawala wa sheria unanawiri nchini.

  • Tags

You can share this post!

Wahalifu mtandaoni kuchukuliwa hatua – Matiang’i

Matiang’i ausifu ukumbi wa kisasa wa Mwai Kibaki...

T L