• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Ababu aomba CAF irejeshe Harambee Stars dimba la AFCON 2023

Ababu aomba CAF irejeshe Harambee Stars dimba la AFCON 2023

WAZIRI wa Michezo Ababu Namwamba jana Jumatatu aliomba Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) lishauriane na lile la Afrika (CAF) ili Harambee Stars irejeshwe kushiriki mchujo wa Taifa Bingwa Afrika (AFCON) 2023.

Namwamba alisema yaliyofanya Stars kuondolewa kwenye mchujo sasa yamepitwa na wakati tangu marufuku ya muda dhidi ya Kenya yaondolewe.

Alisema itakuwa vyema iwapo Kenya itaruhusiwa mara nyingine kushiriki mechi hizo.

Kenya ilikuwa imejumuishwa katika droo ya Afcon 2023 lakini wakaondolewa kutokana na marufuku hiyo, ambayo ilidumu kutoka Februari hadi Novemba 2022.

“Kwa kuwa Fifa na Caf wako hapa, tunaomba tupewe nafasi nyingine ili Harambee Stars ishiriki mchujo wa 2023,” alisema Namwamba.

“Hata timu yetu ya wanawake ingefuzu kushiriki Kombe la Dunia iwapo hatungefungiwa nje kutokana na marufuku ya Fifa,” akaongeza.

“Nina imani kuwa Fifa na Caf watatathmini mazingira ambayo yalisababisha tutimuliwe mchujo, na kutenda haki. Tunawaomba wasihukumu timu kwa kuitoza faini. Haya ni baadhi ya mapendekezo ambayo FKF inastahili kuwasilisha kwa Fifa na Caf,” Waziri alieleza.

Waziri huyo alikuwa akizungumza katika afisi zake kwenye jengo la Maktaba Kuu mtaa wa Upper Hill, Nairobi, baada ya kukutana na maafisa wa Caf na Fifa ambao wapo nchini kwa ziara ya siku mbili.

Ziara hiyo inalenga kutathmini hali ya soka nchini na kuamua hatima ya FKF.

Ujumbe huo unaongozwa na Mkurugenzi wa Fifa anayehusika na masuala ya Afrika na mwanasoka wa zamani, Gelson Fernandes. Wengine ambao walikuwepo ni Noda Nodar Akhalkatsi, Solomon Mudege, Alessandro Gramalgia na Sara Solemale.

Kwenye droo, Harambee Stars ilikuwa katika kundi C pamoja na Cameroon, Namibia na Burundi. Walistahili kuchuana na Burundi mnamo Mei 21 kabla ya kuvaana na Cameroon na Namibia Juni 4 na 8.Mechi za raundi ya tatu za makundi zinastahili kuanza Machi 20 hadi Machi 28.

Fainali hizo zilisongeshwa kutoka Juni 2023 hadi Januari 2024 kutokana na shauku kuhusu hali ya hewa kule Ivory Coast.

Hata hivyo, afisa wa kisheria wa Caf, Nadim Magdy, ambaye pia alikuwepo kikao cha jana Jumatatu alisema ombi la Kenya litazingatiwa baada ya kuwasilishwa kwao rasmi.

  • Tags

You can share this post!

Fainali za Elijah Lidonde kuchezwa Ijumaa ugani Bukhungu

Washukiwa 5 wazuiliwa kwa mauaji ya Chiloba

T L