• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
ADAK yapiga Wakenya 20 marufuku kwa kudaiwa kutumia dawa za kusisimua misuli

ADAK yapiga Wakenya 20 marufuku kwa kudaiwa kutumia dawa za kusisimua misuli

Na AYUMBA AYODI

SHIRIKA la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini Kenya (ADAK) limepiga marufuku wanamichezo 20 kwa kuenda kinyume na sheria za zinazokataza uovu huo.

Mtimkaji wa mbio za mita 100 anayeinuka kwa haraka Samuel Imeta, mshindi wa medali ya fedha ya mbio za 3,000m ya Riadha za Dunia za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 Zena Jemutai na bingwa wa Afrika wa 800m Jarinter Mawia ni baadhi ya walionaswa.

Pia kuna mtimkaji wa mbio fupi na masafa marefu Evangeline Makena, mshindi wa Kip Keino Classic Continental Tour mbio za 400m kuruka viunzi Hannah Mwangi, mbio za 400m Gladys Nthenya Musyoki na mshiriki wa mbio ndefu Agnes Mumbua.

Mnamo Januari 2023, ADAK ilichapisha orodha ya wanamichezo 20 waliopigwa marufuku kwa muda kwa kupatikana upande mbaya wa sheria. Walitoka katika fani za riadha, soka, judo na utunishaji misuli.

Orodha mpya ya walionaswa inajumisha wanariadha, raga na unyanyuaji uzani.

Kutoka riadha kuna Imeta, Bernard Cheruiyot Chepkwony, Victor Koskey, Collins Koros, Amos Kiprotich, Stephen Kipchirchir Kiplagat, Eric Kiptoo, John Kariuki Gikonyo na Cynthia Kendi.

Bingwa wa Afrika Mashariki na mshindi wa zamani wa ututumuaji wa misuli Rashid Issa amepigwa marufuku kwa kukataa kuwasilisha sampuli zipimwe naye mwanaraga Elphas Emong na mchezaji wa mpira wa vikapu David Yamo walipatikana kutumia dawa za aina ya cannabinoid.

Imeta aligunduliwa kutumia dawa za AAS (anabolic-androgenic steroids) wakati wa mashindano ya pili ya Shirikisho la Riadha Kenya mnamo Februari 24 ugani Nyayo.

Alikamilisha mbio za 100m kwa sekunde 9.94 akimfuata mshindi Ferdinand Omanyala aliyeandikisha 9.81, lakini muda yao haikurasimishwa kwa sababu ya hitilafu ya kimitambo.

Imeta alikamata nafasi ya nne nyuma ya Omanyala, ambaye pia alitwaa mataji ya mashindano ya Afrika Kusini (ASA) Grand Prix 1 na Grand Prix 2 mwezi Aprili.

Hata hivyo, Imeta alishinda ASA Grand Prix 3 kwa 10.12 kabla ya kuingia Botswana alikotawala fainali ya pili ya 100m kwa 10.10 wakati wa Botswana Golden Grand Prix. Omanyala aliibuka mshindi wa fainali ya kwanza jijini Gaborone, Botswana kwa 9.78.

Imeta alishirikiana na Omanyala, Boniface Mweresa na Stephen Ochieng kushinda 4x100m kupokezana vijiti kwa 38.26 na kukamata nafasi ya 12 duniani na katika nafasi nzuri ya kufuzu kushiriki Riadha za Dunia jijini Budapest, Hungary.

Marufuku dhidi ya Imeta inamaanisha kuwa matokeo ya 4x100m yako hatarini kufutwa.

Jemutai, ambaye alimaliza mbio za 3,000m katika nafasi ya tano katika Riadha za Dunia U-20 mwaka 2022, alipatikana na dawa zilizopigwa marufuku za Triamcinolone acetonide katika sampuli yake iliyochukuliwa wakati wa mbio za nyika za kitaifa Januari 21, 2023.

Jemutai alimaliza mbio za kilomita 10 katika nafasi ya tatu wakati wa mashindano hayo kabla ya kukamata nafasi ya tatu kwenye Sirikwa Cross Country Classic mnamo Februari 4.

Mawia aligunduliwa nje ya mashindano kwa sampuli zake zilizokusanywa Novemba na Desemba 2022. Sampuli hizo zilipatikana na dawa ya kusisimua misuli ya EPO.

Makena alipimwa wakati wa duru ya tatu na nne za AK mijini Thika na Mombasa mwezi Machi mwaka huu. Dawa za aina ya prednisone, prednisone na triamcinolone acetonide zilipatikana katika katika sampuli zake.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE 

  • Tags

You can share this post!

Manchester City watandika Manchester United na kujizolea...

Ulinzi Starlets mbioni kutetea ubingwa wa Kombe la FKF

T L