• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:03 PM
AFC Leopards wala njama kuzamisha Kakamega Homeboyz

AFC Leopards wala njama kuzamisha Kakamega Homeboyz

NA JOHN ASHIHUNDU

KUNA kila dalili kwamba Kakamega Homeboyz watajipata kwenye hali ya hatari Jumamosi watakapokutana na AFC Leopards katika nusu-fainali ya michuano ya Mozzart Bet Cup ugani Nyayo.

Katika nusu-fainali nyingine, watetezi wa FKF-PL Tusker watakutana na Ulinzi Stars mapema uwanjani humo.

Mwenyekiti wa Homeboyz, Cleophas Shimanyula amekuwa akirusha maneno ya kujigamba kwenye vyombo vya habari akidai kwamba vijana wake wako kwa ubora wa hali ya juu na tayari kuangamiza Ingwe ambao alidai kiwango chao kipo chini kwa sasa.

Shimanyula aliwatahadharisha mashabiki wa Leopards “walio na matatizo ya mshtuko wa moyo wahakikisha wamemeza dawa zao mapema ili kuepuka kupoteza maisha yao kwa kutoamini kitakachotokea uwanjani.”

Lakini akizungumza kuhusu matamshi hayo, kocha Patrick Aussems wa Leopards ametoa onyo kali kwa kiongozi huyo akisema kikosi chake kipo imara kukabiliana na Homeboyz katika mechi hiyo itakayoanza saa tisa alasiri.

“Homeboyz lazima ipambane vikali kuliko ilivyocheza dhidi ya Kariobangi Sharks kwenye mechi ya robo-fainali na kuibuka na ushindi wa 6-2 ugani MISC Kasarani. Iwapo watazembea, tutawaadhibu vikali mbele ya mashabiki wengi wanaotarajiwa kuhudhuria mechi hii.”

Leopards walifuzu baada ya kuitandika Bandari FC 3-0 kwenye robo-fainali nyingine iliyochezewa uwanjani humo.

“Tunalenga ushindi na baadaye ubingwa ili tushiriki katika michuano ya CAF msimu ujao kuwania mamilioni ya pesa mezani. Wachezaji wako na uchu wa ushindi, na kila mtu ako tayari kucheza,” ameongeza Aussems anayetarajiwa kufanya mabadiliko machache

Leopards ilishiriki kwa mara ya mwisho katika michuano ya CAF mnamo 1917, lakini ikatolewa katika raundi ya kwanza na klabu ya FOSSA Junior ya Madacascar kutokana na bao la ugenini

Kwa upande mwingine, kocha Patrick Odhiambo amerekebisha makosa madogo yaliyosababishwa timu yake kushindwa katika mechi mbili za ligi kuu zilizopita dhidi Tusker FC na Nzoia Sugar zilizoshinda kwa 1-0 na 2-0 mtawaliwa. “Kambini morali iko juu na tunaenda uwanjani kushinda,” alisema Odhiambo.

Washindi wa Mozzart Bet Cup wataondoka na Sh2 milioni, timu ya pili itapokea Sh1 milioni, timu ya tatu Sh750,000 huku itakayomaliza ya nne ikipata Sh500,000.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Skonzi zilizotiwa zabibu kavu

Viungo maalum vya nyama vinateka soko moto

T L