• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 3:24 PM
AFCON: Misri wazamisha Morocco na kuingia nusu-fainali itakayowakutanisha na wenyeji Cameroon

AFCON: Misri wazamisha Morocco na kuingia nusu-fainali itakayowakutanisha na wenyeji Cameroon

Na MASHIRIKA

NYOTA Mohamed Salah alifunga bao na kuchangia jingine katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Misri dhidi ya Morocco katika muda wa ziada kwenye robo-fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Jumapili.

Sofiane Boufal aliwaweka Morocco kifua mbele kupitia penalti katika dakika ya sita baada ya Ayman Ashraf kumchezea Achraf Hakimi visivyo.

Hata hivyo, Salah alisawazisha mambo katika dakika ya 53 baada ya kipa Yassine Bounou kutema mpira na kufanya mechi hiyo kuingia muda wa ziada.

Salah ambaye ni fowadi wa Liverpool alichangia bao la pili la Misri lililofumwa wavuni na Mahmoud Trezeguet wa Aston Villa katika dakika ya 100.

Misri wanaonolewa na kocha Carlos Queiroz sasa watavaana na wenyeji Cameroon katika nusu-fainali itakayochezewa jijini Yaounde mnamo Februari 3, 2022.

Misri ambao ni mabingwa mara saba wa Afrika watalazimika kusakata mechi hiyo wakitegemea huduma za kipa chaguo la tatu, Mohamed Abou Gabaski katikati ya michuma. Hii ni baada ya mlinda-lango chaguo la pili, Mohamed Sobhi kupata jeraha akizua fataki ya Nayef Aguerd.

Morocco walikuwa wakiwania fursa ya kunogesha nusu-fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu 1988.

Salah amehusika katika asilimia 64 ya mabao yanayojivuniwa na Misri kwenye AFCON. Amepachika wavuni magoli tisa kati ya 14 tangu awajibishwe na Misri kwa mara ya kwanza kwenye kipute hicho mnamo 2017.

Mechi kati ya Misri na Morocco ilirejesha kumbukumbu za miaka mitano iliyopita ambapo Misri walitandika Morocco 1-0 katika robo-fainali za AFCON 2017 jijini Port-Gentil, Gabon.

Misri ambao ni mabingwa mara saba wa soka ya Afrika walihitaji penalti 5-4 mnamo Januari 26, 2022 ili kudengua wafalme mara mbili, Ivory Coast, kwenye hatua ya 16-bora baada ya kuambulia sare tasa chini ya dakika 120 jijini Douala.

Atlas Lions wa Morocco walilazimika kutoka nyuma na kupokeza Malawi kichapo cha 2-1 kwenye mechi ya raundi ya muondoano iliyowakutanisha jijini Yaounde mnamo Januari 25, 2022.

Morocco walijibwaga ulingoni wakipigiwa upatu wa kushinda ikizingatiwa ubora wa rekodi yao dhidi ya Misri. Walikuwa wameshinda michuano 14 na kuambulia sare mara 12 kutokana na mechi 29 za awali kati yao na Pharaohs wa Misri.

Miamba hao walikutana mara ya mwisho mnamo Agosti 2017 katika pambano la kufuzu kwa fainali za Kombe la CHAN 2018 zilizofanyika Morocco. Misri walipokezwa kichapo cha 3-1 katika marudiano ya mashindano hayo baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza.

Misri walikosa huduma za kipa mzoefu chaguo la kwanza Mohamed El-Shennawy kutokana na jeraha alilopata dhidi ya Ivory Coast. Morocco kwa upande wao walikuwa bila Ilias Chair aliyeumia wakati wa mchuano wa mwisho wa Kundi C uliokamilika kwa sare ya 2-2 dhidi ya Gabon mnamo Januari 18, 2022.

Huku Misri wakifukuzia taji la nane la AFCON, Morocco walikuwa na kiu ya kumaliza ukame wa miaka 45 tangu watawazwe wafalme kipute hicho mnamo 1976 nchini Ethiopia. Walifungua kampeni za Kundi C kwa kupepeta Ghana 1-0 kabla ya kulaza Comoros 2-0 na kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Gabon. Misri walianza kampeni za Kundi D kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Nigeria kabla ya kutandika Guinea-Bissau na Sudan 1-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

UDA walalama Ford Kenya inawahujumu

Kocha Vihiga Queens asema hakuna kulaza damu Ligi Kuu

T L