• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
UDA walalama Ford Kenya inawahujumu

UDA walalama Ford Kenya inawahujumu

NA BRIAN OJAMAA

WAWANIAJI wa viti tofauti kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kaunti ya Bungoma, wanamuomba Naibu Rais William Ruto kuchukua hatua kuzima mizozo inayoibuka katika chama hicho baada ya kuungana na ANC na Ford Kenya.

Wawaniaji hao kutoka maeneo bunge yote tisa ya kaunti hiyo wanalalamikia wanachotaja kama hujuma kutoka kwa washirika wengine katika muungano wa Kenya Kwanza Alliance.

Wakihutubia wanahabari mjini Bungoma Jumamosi, siku moja baada ya Muungano wa Kenya Kwanza Alliance kuzuru kaunti hiyo kwa mara ya kwanza, viongozi wa mashinani wa UDA walisema wanahuzunishwa na hali ilivyobadilika katika mkutano uliofanyika uwanja wa Posta.

Wakiongozwa na wawaniaji wa unaibu gavana Bi Sophy Nekoye Waliaula, mwaniji wa kiti cha Mwakilishi wa Kike Bi Maria Nato, mwaniaji wa kiti cha eneobunge la Kanduyi Bw Mulunda Khaoya na mwaniaji wa udiwani wa wadi ya Malondo Magharibi Bw Zebedee Amos Wangila, walilalamika kwamba walinyanyaswa na kutengwa na viongozi wengine wa OKA.

“Tunataka kukutana na kiongozi wa chama chetu Dkt William Ruto, juhudi zetu haziwezi kukosa kutambuliwa, tumetumia pesa zetu, tumewekeza muda na nguvu katika juhudi zetu za kujenga chama hicho, hatuwezi kukubali kukipoteza kwa sababu ya kubuniwa kwa muungano ambao utatufanya tuzimwe,” alisema Bi Nekoye.

Aliwahimiza wawaniaji wa UDA kusimama imara na kuhakikisha wanakutana na kiongozi wa chama kutatua masuala tata.

Bi Nato alimuomba Dkt Ruto kuhakikisha kuwa hawatatengwa kwa sababu ya muungano huo mpya.

“Umekuwa ukituhakikishia katika mikutano kadhaa kwamba hakuna kutengewa maeneo kwa kuwa baadhi yetu tutaumia, heshimu hilo ili nasi tuweze kuokoa maisha yetu ya kisiasa,” alisema.

Bi Nato aliwataka viongozi wengine wa UDA kukomesha ubaguzi na kuruhusu wawaniaji wengine kukua badala ya kuendesha siasa chafu zinazoweza kusababishia chama hasara eneo la Magharibi.

“Mwaniaji wetu wa kiti cha ugavana Zachariah Baraza na wawaniaji wengine muhimu wa UDA hawakutambuliwa licha ya kuwa walitekeleza jukumu muhimu kujenga chama na kupanga mkutano huo ukafaulu, tulipuuzwa kabisa,” alisema.

Bw Mulunda Khaoya alikitaka chama kuwapa wawaniaji wote nafasi sawa ya kushindana.

“Hakuna chama kilicho muhimu kuliko kingine, ruhusu wawaniaji wa vyama vyote kushiriki katika uchaguzi ili wapigakura wachague kiongozi aliye bora,” alisema.

Alilaumu baadhi ya wabunge wa UDA kwa kutowatambua wawaniaji licha ya kwamba walitekeleza jukumu muhimu kufanikisha mkutano huo.

“Tunamshukuru mbunge wa Sirisia John Walukhe kwa juhudi zake kuhakikisha mwaniaji wetu wa ugavana alitambuliwa, wengine wetu tulipuuzwa, tulihujumiwa kabisa, hatutakubali Ford Kenya kututumia,” alisema.

Katika mkutano huo, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na viongozi wengine walimtaja Spika wa Seneti

Ken Lusaka anayegombea kiti cha useneta mara nyingi kuliko Baraza aliyehudhuria hafla hiyo jambo ambalo lilikasirisha wanachama wa UDA kaunti ya Bungoma.

You can share this post!

Familia yatoa wito mshukiwa ashtakiwe humu nchini

AFCON: Misri wazamisha Morocco na kuingia nusu-fainali...

T L