• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
AFCON: Senegal yazamisha Burkina Faso na kuingia fainali

AFCON: Senegal yazamisha Burkina Faso na kuingia fainali

Na MASHIRIKA

SENEGAL walifuzu kwa fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) baada ya kukomoa Burkina Faso 3-1 mnamo Jumatano usiku nchini Cameroon.

Fowadi Sadio Mane wa Liverpool alipachika wavuni bao la tatu la Senegal na kufikia rekodi ya Henri Camara aliyekuwa mfungaji bora wa muda wote wa Lions of Teranga kwa magoli 29.

Teknolojia ya VAR ilinyima Senegal penalti mbili huku kipa wa Burkina Faso, Herve Koffi akipata jeraha katika kipindi cha kwanza.

Abdou Diallo na Idrissa Gueye walifungulia Senegal ukurasa wa mabao katika dakika za 70 na 76 mtawalia kabla ya Burkina Faso kurejea mchezoni kupitia kwa fowadi Blati Toure.

Senegal wanaoshikilia nafasi ya kwanza Afrika na ya 20 duniani, sasa watamenyana ama na Misri au wenyeji Cameroon kwenye fainali itakayosakatiwa uwanjani Olembe mnamo Februari 6, 2022.

Burkina Faso sasa watachuana ama na Misri au Cameroon kwenye gozi la kutafuta mshindi nambari tatu au nne mnamo Februari 5, 2022.

“Matokeo haya yanaridhisha. Tulianza kampeni za AFCON kwa kusuasua, lakini kikosi kimekuwa kikiimarika hatua kwa hatua. Ni muhimu zaidi tukiendeleza msukumo huu ambao tumeshuhudia hadi mwisho kipute na kutwaa taji,” akasema Mane.

Kwa upande wake, kocha Aliou Cisse wa Senegal amesema uthabiti unaojivuniwa na kikosi chake unawaweka nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa wa makala ya 33 ya AFCON mwaka huu.

Wanafainali hao wa 2002 na 2019 walifuzu kwa hatua ya nne-bora ya kipute hicho mnamo Januari 30, 2022 baada ya kutandika Equatorial Guinea 3-1 katika uwanja wa Omnisport de Douala, Cameroon.

“Ushindi dhidi ya Burkina Faso unatuweka katika uhalisia wa kutwaa taji la AFCON. Japo tulianza kampeni kwa matao ya chini, mashabiki wetu sasa wana kila sababu ya kutarajia makuu. Hatutapoteza dira kwa kuwa kipute kimeingia hatua muhimu nay a kusisimua zaidi,” akasema Cisse.

Senegal walifungua kampeni zao za Kundi B kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Guinea na Malawi. Waliingia robo-fainali baada ya kupepeta Cape Verde 2-0 katika hatua ya 16-bora.

Burkina Faso wanaoshikilia nafasi ya 60 kimataifa, wameshinda mechi zote za robo-fainali za AFCON, zikiwemo tatu kutokana na makala manne yaliyopita. Walikomoa mabingwa wa 2004, Tunisia, kwa bao 1-0 kwenye robo-fainali baada ya kudengua Gabon kwa penalti 7-6 katika raundi ya 16-bora.

Kikosi hicho kilifungua kampeni za Kundi A kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Cameroon kabla ya kutandika Cape Verde 1-0 na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Ethiopia waliotawazwa wafalme mnamo 1962 jijini Addis Ababa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Moto waua watu 5 wakiwemo jamaa 3

Barcelona wathibitisha kumsajili Aubameyang bila ada yoyote

T L