• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Barcelona wathibitisha kumsajili Aubameyang bila ada yoyote

Barcelona wathibitisha kumsajili Aubameyang bila ada yoyote

Na MASHIRIKA

BARCELONA wamethibitisha kumsajili fowadi Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Arsenal bila ada yoyote.

Nyota huyo raia wa Gabon mwenye umri wa miaka 32, alitia saini mkataba aliopokezwa na Barcelona mnamo Januari 31, 2022 ila tukio hilo likatangazwa rasmi na miamba hao wa Uhispania mnamo Februari 2, 2022.

Kandarasi ya sasa kati ya Aubameyang na Barcelona inatarajiwa kukatika Juni 30, 2025 japo kikosi hicho kitakuwa huru kumwachilia mvamizi huyo kutafuta hifadhi mpya kwingineko mnamo Juni 2023 iwapo hataridhisha kambini mwao. Kikosi kitakachowania maarifa yake wakati huo kitalazimika kuweka mezani Sh12.5 bilioni.

“Najivunia kuwa hapa. Lengo langu kwa sasa ni kusaidia Barcelona kurejea katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA),” akasema Aubameyang.

Akiwa Arsenal, sogora huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alipachika wavuni mabao 92 kutokana na mechi 163. Hakuwahi kuchezea Arsenal tangu Disemba 2021 alipokiuka kanuni za kinidhamu na kuvuliwa utepe wa unahodha ambao fowadi Alexandre Lacazette alipokezwa.

Arsenal walimsajili Aubameyang kwa Sh8.4 bilioni mnamo Januari 2018 kutoka Dortmund ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AFCON: Senegal yazamisha Burkina Faso na kuingia fainali

Raila asema ukombozi wa tatu na wa kufufua uchumi umeanza

T L