• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Arsenal warejea kileleni mwa jedwali la EPL

Arsenal warejea kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL walirejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumanne usiku baada ya kupepeta Chelsea 3-1 ugani Emirates.

Matokeo hayo yalirejesha matumaini finyu ya Arsenal kutawazwa mabingwa wa EPL msimu huu licha ya presha kali kutoka kwa mabingwa watetezi Manchester City.

Hadi walipoangusha Chelsea, vijana hao wa kocha Mikel Arteta hawakuwa wameshinda mechi nne mfululizo na walikuwa wamepokezwa kichapo cha 4-1 na Man-City waliowang’oa kileleni mnamo Aprili 30, 2022 baada ya kutandika Fulham 2-1.

Wakicheza dhidi ya Chelsea, Arsenal waliwekwa kifua mbele na nahodha Martin Odegaard aliyefunga mabao mawili kunako dakika za 18 na 31 mtawalia. Gabriel Jesus alipachika wavuni bao la tatu la Arsenal katika dakika ya 34 kabla ya Noni Madueke kufuta machozi ya Chelsea katika dakika ya 65.

Kichapo kutoka kwa Arsenal kilikuwa cha sita mfululizo kwa Chelsea kupokezwa chini ya kocha mshikilizi wa mikoba yao, Frank Lampard. Arsenal wangalifunga mabao zaidi katika kipindi cha pili ila juhudi za wavamizi wao zikazimwa na kipa Kepa Arrizabalaga aliyejituma vilivyo.

Arsenal sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 78 baada ya kusakata jumla ya michuano 34. Pengo la pointi mbili linawatenganisha na nambari mbili Man-City ambao wana michuano miwili zaidi ya akiba. Chelsea kwa upande wao wanashikilia nafasi ya 12 kwa alama 39 baada ya mechi 33.

Ilivyo, Arsenal sasa wanahitajika kushinda mechi zao zote nne zilizosalia ligini muhula huu na kutarajia Man-City wapoteze angalau michuano miwili kati ya sita ili watie kibindoni ufalme wa EPL kwa mara ya kwanza tangu 2003-04.

Sawa na Chelsea waliopigwa na Brentford 2-0 katika pambano lao la awali ligini, Arsenal nao walikuwa na kibarua kizito cha kujinyanyua baada ya Man-City kuwatandika 4-1 uwanjani Etihad, Jumatano iliyopita.

Matokeo hayo pamoja na sare tatu dhidi ya Liverpool, West Ham United na Southampton, yalididimiza zaidi matumaini ya Arsenal kuibuka mabingwa wa EPL msimu huu japo tayari wamefuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza tangu 2016-17.

Mechi dhidi ya Chelsea ilikuwa ya saba mfululizo kushuhudia Arsenal wakifunga bao nao wakikubali kuokota mpira kimiani. Sasa wamepachikwa jumla ya magoli 12 kutokana na mechi tano zilizopita. Hata hivyo, ni Newcastle pekee ambao wamenyima Arsenal fursa ya kufunga bao uwanjani Emirates muhula huu.

Japo Chelsea wanapigiwa upatu wa kumsajili mkufunzi Mauricio Pochettino mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23, Lampard ameshuhudia kikosi chake kikiweka historia mbovu ya kupoteza jumla ya mechi 20 katika msimu mmoja, kwa mara ya kwanza tangu 1987-88.

Chelsea sasa hawajashinda mechi yoyote kati ya tisa zilizopita tangu aliyekuwa mkufunzi wao, Graham Potter, awaongoze kupepeta Leicester City 3-1 mnamo Machi 2023. Hofu zaidi kwa miamba hao wa zamani waliotawazwa wafalme wa EPL 2016-17, ni kwamba wamefunga sasa mabao mawili pekee – dhidi ya Arsenal na Brighton waliowapiga 2-1, tangu Lampard apokezwe upya mikoba yao mwanzoni mwa Aprili 2023.

Isitoshe, wameshinda mechi moja pekee kati ya 10 zilizopita katika EPL ugenini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mvulana aokoa wenzake baada ya dereva wa basi kuzirai

PSG wamsimamisha Lionel Messi kazi kwa muda wa wiki mbili...

T L