• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
PSG wamsimamisha Lionel Messi kazi kwa muda wa wiki mbili na kumtoza faini

PSG wamsimamisha Lionel Messi kazi kwa muda wa wiki mbili na kumtoza faini

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, amesimamishwa kazi kwa muda wa wiki mbili na Paris Saint-Germain (PSG) baada ya kusafiri hadi Saudi Arabia bila idhini ya waajiri wake.

Messi alifunga safari hiyo baada ya PSG kupokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Lorient katika mchuano ulioshuhudia Messi akiwajibishwa kwa dakika zote 90 uwanjani Parc des Princes.

Messi sasa hatashiriki mazoezi au kuchezea PSG katika mechi yoyote katika kipindi hicho cha adhabu.

Inaaminika kwamba Messi, 35, alikuwa amewaomba PSG idhini ya kumruhusu kutua Saudi Arabia kufanya shughuli zake binafsi za kibiashara ila akanyimwa nafasi hiyo na waajiri wake.

Kwa mujibu wa sogora huyo wa zamani wa Barcelona, alikuwa awali amekubaliwa kusafiri hadi Saudi Arabia kabla ya idhini hiyo safari yake kupigwa marufuku kutokana na mabadiliko kwenye ratiba ya mazoezi ya PSG.

Messi ambaye pia ametozwa faini na PSG, ana jukumu jingine la kuwa balozi wa utalii nchini Saudi Arabia.

Mkataba wa miaka miwili kati ya PSG na fowadi huyo aliyeongoza Argentina kushinda Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23.

Mnamo Machi, Naibu rais wa Barcelona, Rafael Yuste, alifichua kwamba walikuwa katika mazungumzo ya kumshawishi Messi kurejea kambini mwao mwishoni mwa muhula huu.

Messi amefungia PSG jumla ya mabao 31 na kuchangia 34 mengine kutokana na mechi 71 ambazo amechezea PSG waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo 2021-22.

Adhabu ambayo amepokezwa na PSG itamnyima fursa ya kucheza dhidi ya Troyes na Ajaccio kadri waajiri wake wanavyopania kuhifadhi taji la Ligue 1. Kufikia sasa, wanajivunia pengo la alama tano kileleni mwa jedwali zikisalia mechi tano pekee kwa kampeni za ligi msimu huu kukamilika rasmi. PSG wanapigiwa upatu wa kunyanyua taji la Ligue 1 kwa mara ya tisa katika kipindi cha misimu 11.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Arsenal warejea kileleni mwa jedwali la EPL

Sociedad wazima kabisa matumaini finyu ya Real Madrid...

T L