• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
AUSTRALIAN OPEN: Mwanatenisi Medvedev atoka nyuma na kuangusha Krajinovic

AUSTRALIAN OPEN: Mwanatenisi Medvedev atoka nyuma na kuangusha Krajinovic

Na MASHIRIKA

KOCHA Gilles Cervara anayemtia makali mwanatenisi Daniil Medvedev wa Urusi, aliondoka uwanjani kwa hasira baada ya mchezaji huyo kupoteza uongozi wa seti mbili kwenye raundi ya tatu ya michuanoya Australian Open mnamo Februari 13.

Hata hivyo, nyota huyo alitoka chini na kuibuka mshindi wa mechi hiyo kati yake na Filip Krajinovic baada ya kutawala seti tatu za mwisho kati ya tano za 6-3, 6-3, 4-6, 3-6 na 6-0.

Matokeo ya seti ya pili yakiwa 4-1, Cervara alikurupuka kwenye eneo la makocha, akapiga unyende kwa mseto wa lugha tatu tofauti – Kiingereza, Kifaransa na Kirusi kisha kutwaa begi lake na kuondoka kabisa bila ya kurejea uwanjani.

“Ndimi pekee niliyeelekewa maneno aliyoyataja kabla ya kuondoka uwanjani. Alisema anataka kuondoka ili niwe mtulivu. Kwamba alihisi kuwepo kwake pale uwanjani nikicheza kulinitia hofu na presha ya kufanya vyema. Kweli alipotoka nilitulia na nikambwaga mpinzani wangu kirahisi kwenye seti tatu za mwisho,” akasema Medvedev kwa kukiri kwamba kamera zilizokuwa zikimulika kila mpira alioupakua pia zilimnyima nafasi ya kumakinika ipasavyo.

Medvedev ni miongoni mwa wanatenisi wanaopigiwa upatu wa kumpokonya bingwa mtetezi Novak Djokovic ufalme wa Australian Open mwaka huu.

Medvedev amepangiwa kukutana na Mackenzie McDonald hapo Jumapili baada ya mwanatenisi huyo raia wa Amerika kumpokeza Lloyd Harris wa Afrika Kusini kichapo cha seti 7-6 (9-7) 6-1, 6-4.

Stefanos Tsitsipas pia alifuzu kwa raundi ijayo baada ya kumzamisha Mikael Ymer wa Uswidi kwa seti 6-4, 6-1, 6-1. Kwingineko, Casper Ruud aliweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Norway baada ya baba yake, Christian kutinga raundi ya nne ya tenisi za Grand Slam.

Ruud alimpokeza Radu Albot wa Moldova kichapo cha seti 6-1, 5-7, 6-4, 6-4 na kujikatia tiketi ya kuvaana na mshindi wa mechi nyingine ya raundi ya tatu kati ya Andrey Rublev wa Urusi na Feliciano Lopez wa Uhispania. Babaye Ruud aliwahi kutinga raundi ya nne ya tenisi za Australian Open mnamo 1997.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Xhaka amjeruhi Lacazette wakiwa mazoezini kambini mwa...

Otieno ataka Zesco United ijitume zaidi Zambia