• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Barcelona waaga UEFA katika hatua ya makundi baada ya kuzamishwa na Bayern

Barcelona waaga UEFA katika hatua ya makundi baada ya kuzamishwa na Bayern

Na MASHIRIKA

MABINGWA mara tano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Barcelona, walipigwa 3-0 na Bayern Munich mnamo Jumatano usiku na hivyo kudenguliwa kwenye hatua ya makundi ya kipute hicho kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 17.

Barcelona hawajawahi kukosa kunogesha kampeni za UEFA katika hatua ya 16-bora tangu 2003-04 walipokosa kufuzu kabisa kushiriki kivumbi hicho cha haiba kubwa.

Kubanduliwa kwao mapema kwenye UEFA kuliendeleza masaibu ya miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania ambao sasa wanakabiliwa na panda-shuka tele za kifedha. Changamoto hizo ni sababu kuu ya kuagana kwao na nyota Lionel Messi aliyetua Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa bila ada yoyote mwanzoni mwa msimu huu wa 2021-22.

Barcelona walikuwa na ulazima wa kushinda mechi yao kwa matarajio kwamba Benfica wangezidiwa ujanja na Dynamo Kyiv. Hata hivyo, Benfica kutoka Ureno walikomoa Kyiv nyumbani na kusaza Barcelona ya kocha Xavi Hernandez katika nafasi ya tatu. Miamba hao watalazimika sasa kushiriki raundi ya muondoano kwenye Europa League.

Mechi kati ya Bayern na Barcelona ilichezewa katika mazingira ya theluji tele na haikuhudhuriwa na mashabiki kwa sababu ya kanuni kali za kudhibiti msambao wa virusi vya corona nchini Ujerumani. Bayern walifunga mabao yao kupitia Robert Lewandowski, Leroy Sane na Jamal Musiala.

Bayern wanasonga kwa hatua ya 16-bora wakijivunia rekodi nzuri ya kushinda mechi zao zote za makundi. Benfica walijizolea alama nane huku Barcelona waliofunga mabao mawili pekee kwenye kampeni zote za makundi wakizoa alama saba.

Droo ya Europa League itafanyika Disemba 13 mjini Nyon, Uswisi na Barcelona watamenyana na kikosi kimoja kitakachokamilisha kampeni za makundi katika nafasi ya pili. Rangers kutoka Scotland ni miongoni mwa vikosi hivyo.

You can share this post!

Miheso aokoa Kenya Police, Homeboyz ikipaa kileleni mwa ligi

Mbungo roho juu masogora wake wataliza KCB leo

T L