• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Barcelona wazamisha chombo cha Real Madrid katika El Clasico ugani Camp Nou

Barcelona wazamisha chombo cha Real Madrid katika El Clasico ugani Camp Nou

Na MASHIRIKA

BARCELONA walipepeta Real Madrid 2-1 katika gozi la El Clasico na kufungua mwanya wa alama 12 kati yao na mabingwa hao watetezi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Real walitangulia kuona lango la wenyeji wao kupitia kwa beki wa Barcelona, Ronald Araujo, aliyejifunga mwanzoni mwa kipindi cha kwanza.

Barcelona walisawazishiwa na Sergi Roberto katika dakika ya 45 kabla ya Franck Kessie kupachika wavuni bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Zikisalia mechi 12 pekee kwa kampeni za La Liga msimu huu kukamilika, Barcelona sasa wanadhibiti kilele cha jedwali kwa alama 68 na wanapigiwa upatu wa kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu 2018-19. Real wanakamata nafasi ya pili kwa pointi 56, tano kuliko Atletico Madrid wanaofunga orodha ya tatu-bora.

Barcelona watavaana na Elche katika pambano lao lijalo la La Liga mnamo Aprili 1 ugenini, siku moja kabla ya Real kualika Valladolid ugani Bernabeu.

Real na Atletico Madrid wametamalaki kipute cha La Liga kwa misimu mitatu iliyopita baada ya kupiga kumbo Barcelona ambao sasa wameshinda mechi 22 kati ya 26 zilizopita ligini msimu huu.

Chini ya kocha Xavi Hernandez, miamba hao ambao wamepiga sare mbili na kupoteza michuano miwili, wamefungwa mabao manane pekee ligini msimu huu wa 2022-23.

Barcelona, ambao tayari wametwaa taji la Spanish Super Cup, bado wanafukuzia mataji mawili zaidi msimu huu, likiwemo kombe la Copa del Rey. Walitandika Real 1-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya kipute hicho na watarudiana ugani Camp Nou mwanzoni mwa Aprili2023.

Licha ya kuduwazwa na Almeria kwa kichapo cha 1-0 ligini mwishoni mwa Februari, Barcelona sasa wameshinda mechi tatu zilizopita za La Liga – walikomoa Valencia 1-0 kabla ya kusajili ushindi sawa na huo dhidi ya Athletic Bilbao.

Barcelona tayari wamejizolea alama 35 kutokana na mechi 13 baada ya kuweka rekodi ya kushinda mechi 11 na kupoteza mbili pekee.

Sawa na Barcelona, Real pia wanapigania mataji matatu msimu huu na tayari wamefuzu kwa robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Chelsea baada ya kudengua Liverpool kwa jumla ya mabao 6-2 katika hatua ya 16-bora.

Real walipoteza dhidi ya Mallorca mwanzoni mwa Februari, kabla ya kutoshana nguvu na Atletico na Real Betis kisha kukomoa Espanyol 3-1 ugani Bernabeu wikendi iliyopita.

Hadi walipoangushwa na Barcelona, Real walikuwa na rekodi nzuri katika mechi za ugenini msimu huu huku wakijizolea alama 28 kutokana na mechi 13 na kushinda Barcelona mara tano kati ya sita zilizopita ligini. Barcelona nao hawakuwa wameshinda Real ugani Camp Nou tangu Oktoba 2018 na walipoteza 3-1 dhidi ya miamba hao mwanzoni mwa msimu huu ugani Bernabeu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa selimundu wasababishia familia...

Wito kwa wanahabari waangazie maswala muhimu kuhusu afya,...

T L