• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa selimundu wasababishia familia dhiki

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa selimundu wasababishia familia dhiki

NA PAULINE ONGAJI

KWA miaka 16 sasa, maisha yake Derrick Otieno, mwanafunzi wa kidato cha nne hapa jijini Nairobi, yamejawa na dhiki.

Hii ni kwa sababu mvulana huyu wa miaka 17 amekuwa akiishi na maradhi ya selimundu (sickle cell), ugonjwa uliogundulika akiwa na mwaka mmoja pekee.

Mamake Otieno, Bi Kerine Onyango asema kwamba kutokana na maradhi haya, maisha yao yamejaa changamoto nyingi.

“Kwanza kabisa, mwanangu hukumbwa na matatizo ya kiafya kama vile udhaifu, macho kugeuka na kuwa manjano, maumivu ya kichwa na viungo, na hata wakati mwingine kuendesha.”

Ni hali ambayo imemsababishia unyanyapaa.

“Kila wakati analazimika kwenda hospitalini, na matatizo ya kiafya yameathiri uzani wake. Hiki kimekuwa kichocheo kikubwa cha ubaguzi miongoni mwa wenzake,” aeleza.

Lakini, kwa Bi Onyango, tatizo kuu zaidi limekuwa kugharimia matibabu ya ugonjwa huu hasa ikizingatiwa kwamba pesa nyingi zinahitajika kudhibiti maradhi haya.

“Sharti nihakikishe lishe bora ambapo daktari anapendekeza kwamba chakula chake lazima kijumuishe vile vilivyo na viwango vya juu vya madini ya chuma kama vile maini, matunda, spinachi na mboga za kiasili, ambavyo ni ghali,” aeleza.

Kisha kuna matibabu ambapo Bi Onyango asema kila siku lazima atumie angaa Sh4,000 kununua dawa ambazo zinahusisha Hydroxyurea, Folic acid, Penicillin V na Neurobin, zinazotumika kudhibiti makali ya maradhi haya.

Gharama hii imekuwa mzigo mzito kwa mama huyu hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa hana kipato thabiti. Alilazimika kuacha ajira kama mwalimu wa shule ya chekechea ili kupata wakati wa kutosha kumshughulikia mwanawe.

“Awali nilikuwa naendesha kituo cha kuwalinda watoto wadogo, wazazi wao wanapoenda kazini, lakini baada ya mkurupuko wa maradhi ya COVID-19 nililazimika kukifunga kwani idadi ya wateja ilipungua.”
Kwa sasa anaendesha shughuli hii nyumbani kwake lakini idadi ya watoto wanaoletwa ni ndogo, kumaanisha kuwa pesa anazopokea hazitoshelezi mahitaji yao.
Kwa upande mwingine, elimu yake Otieno pia imeathirika.

“Tangu ajiunge ana shule ya upili, matatizo ya kiafya yanayotokana na hali hii yaliongezeka ambapo kuna wakati ambao angeathirika hata mara mbili kwa muhula.”

Kwa mfano, Septemba 2022, mvulana huyu alishuhudia athari mbaya zaidi.

“Wakati huo alishindwa kutembea na kula na baadhi ya sehemu za mwili zikabadili rangi na kuwa manjano, ambapo alilazimika kulazwa hospitalini kwa takriban mwezi mmoja na hata kuwekewa painti nane za damu.”

Derrick Dickens Otieno akiwa na mama yake Kerine Onyango nyumbani kwao Ngando, Dagoretti, Kaunti ya Nairobi. PICHA|EVANS HABIL

Hii ilimlazimu Bi Onyango kumbadilisha mwanawe kutoka mwanafunzi wa bweni hadi wa kutwa.

“Alitamani sana kusomea shule ya bweni ambapo alijiunga nayo mwaka wa 2019 baada ya kukamilisha masomo ya msingi,” aeleza.

Lakini wakati huo asema kwamba angepokea simu za mara kwa mara kutoka shuleni, kwa sababu kunao wakati ambapo angezidiwa na ugonjwa hata usiku wa manane.

“Pia, nilikuwa nalazimika kwenda shuleni kila wikendi kumfulia kwani hangeweza jifanyia hivyo.”

Kwa sasa, analazimika kuabiri gari mara nne kila asubuhi anapoenda shuleni.

“Analazimika kuondoka nyumbani saa kumi unusu alfajiri. Hii ina changamoto nyingi kama vile kurauka ambapo kijibaridi cha asubuhi huchochea matatizo haya hata zaidi. Pia, kuna wakati ambapo ni shida kupata nauli,” aeleza Bi Onyango.

Changamoto hizi zote zimeathiri masomo ya mwanafunzi huyu kwani masomo yake yamekuwa yakididimia, suala ambalo pia limemsababishia msongo wa akili.

Maradhi ya selimundu huathiri kati ya watu milioni 20 na 25 duniani kote, kati ya watu milioni 12 na milioni 15 wanaishi barani Afrika.

Kati ya asilimia 75 na asilimia 85 ya watu hawa ni watoto wanaozaliwa barani Afrika. Asilimia hii ni sawa na watoto 240,000. Kati ya asilimia 50 na asilimia 80 hufariki kabla ya kutimu umri wa miaka mitano.

Kutokuwepo kwa utaratibu maalum wa kuchunguza maradhi haya miongoni mwa watoto wanaozaliwa na maradhi haya, vile vile ukosefu wa matibabu maalum, husababisha vifo vya asilimia 50 ya watoto wanaozaliwa na maradhi haya katika mataifa yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara, kabla hawajatimu umri wa miaka mitano.

Nchini Kenya, inakadiriwa kwamba watoto 6,000 huzaliwa wakiwa na maradhi ya selimundu kila mwaka, ambapo wataalamu wanahoji kwamba huenda idadi hii ikaongezeka kufikia mwaka wa 2050 hasa ikizingatiwa kwamba idadi ya watu inatarajiwa pia kuongezeka.

Hapa nchini maradhi haya yamekithiri sana katika kaunti 18 zilizoko katika maeneo ya Magharibi, Nyanza na Pwani ya Kenya. Haya ni maeneo ambapo pia maradhi ya malaria yamekithiri.

Hata hivyo, kwa sababu ya watu kuhama kutoka sehemu moja hadi ingine, vile vile ndoa baina ya watu kutoka sehemu tofauti, hali hii pia imekuwa ikiripotiwa kwa wingi katika maeneo mengine nchini.

Kulingana na Dkt Fredrick Okinyi, Mwenyekiti wa wakfu wa maradhi ya selimundu hapa nchini, watu wanaoishi na maradhi haya hukumbana na changamoto nyingi za kiafya, kumaanisha kuwa wanahitaji matibabu thabiti.

“Athari za kiafya zinazotokana na maradhi haya ni kali sana ambapo zaweza msababisha mgonjwa kukumbwa na shida ya viungo na ongezeko la hatari za mambukizi. Hii huathiri pakubwa hali na maisha ya mwathiriwa,” asema.

Anasema kwamba utambuzi wa mapema ni muhimu ili kuanzisha matibabu thabiti mapema.

“Lakini tatizo ni kwamba Wakenya wengi wanashindwa kumudu gharama za utambuzi na matibabu ya kukabiliana na makali ya maradhi haya. Mambo huwa magumu hata zaidi hasa ikizingatiwa kwamba Bima ya kitaifa ya afya NHIF, haigharamii baadhi ya matibabu muhimu ya maradhi ya selimundu,” aeleza.

Kulingana na Dkt Okinyi, mfano mzuri ni utaratibu wa reticulocyte counts (utaratibu unaotumiwa kutambua idadi na au asilimia ya seli nyekundu za damu zilizoathirika ili kusaidia kutathmini matatizo yanayokumba seli hizi), ambao licha ya kuwa hupunguza gharama za matibabu ya wagonjwa wa selimundu, haugharamiwi katika mpango huu wa bima.

“Kumbuka kwamba utaratibu huu hupunguza matibabu ya maradhi haya kuwa kati ya Sh40,000 na Sh 80,000, na hivyo kuzuia mgonjwa kulazwa hospitalini, ambapo gharama za kulazwa na matibabu yaweza fikia Sh120,000.”

Kulingana na Dkt Okinyi, kutokana na sababu kuwa matibabu ya maradhi haya bado hayajapatikana, basi juhudi zinapaswa kuelekezwa katika udhibiti wa maradhi haya.

“Kwa sasa Kenya haina mwongozo kamili kuhusu udhibiti wa ugonjwa huu. Kunapaswa kuwa na mikakati thabiti ya kufanya hivyo ili kupunguza mzigo wa maradhi ya selimundu miongoni mwa Wakenya,” aeleza.

Profesa Fred Were kutoka chama cha madaktari wa watoto nchini, asema mbali na matibabu, kunapaswa kuwa na kampeni thabiti za uhamasishaji kuhusu maradhi haya.

“Watu wanapaswa kuelimishwa kuhusu maradhi haya, umuhimu wa matibabu ya mapema, vile vile umuhimu wa ushauri wa kijinetiki wakati wa kuchumbiana, kabla ya watu kufunga ndoa,” aeleza.

Aidha anasisitiza kwamba wakati umewadia kwa viongozi kutoka kaunti zilizoathirika pakubwa na maradhi haya, kupaza sauti zao kuhusiana na maradhi haya.

  • Tags

You can share this post!

Rennes wapepeta PSG na kukomesha rekodi ya kutopigwa kwa...

Barcelona wazamisha chombo cha Real Madrid katika El...

T L