• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Bayern wamtema Sadio Mane kikosini kwa sababu ya utovu wa nidhamu

Bayern wamtema Sadio Mane kikosini kwa sababu ya utovu wa nidhamu

Na MASHIRIKA

SADIO Mane hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachowajibishwa na Bayern Munich dhidi ya Hoffenheim katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu huu baada ya kubainika kwamba alimpiga konde fowadi mwenzake, Leroy Sane.

Kwa mujibu wa ripoti nchini Ujerumani, inadaiwa kwamba Mane alimpiga Sane usoni baada ya mchuano wa mkondo wa kwanza robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Aprili 11, 2023 ugani Etihad.

Mechi hiyo ilishuhudia Bayern wakipokezwa kichapo cha 3-0 na hivyo kudidimiza zaidi matumaini yao ya kusonga mbele na kuingia nusu-fainali za UEFA msimu huu.

Kulingana na Bayern, Mane ambaye ni fowadi wa Senegal ametemwa kikosini kwa muda kwa sababu ya “utovu wa nidhamu” na atatozwa faini kubwa.

“Sadio, 31, hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachochezea Bayern dhidi ya 1899 Hoffenheim wikendi hii ugani Allianz Arena. Hii ni kwa sababu ya utovu wa nidhamu aliodhihirisha baada ya mechi dhidi ya Man-City. Pia atatozwa faini,” ikasema sehemu ya taarifa ya Bayern.

Bayern watakuwa wenyeji wa Man-City katika mchuano wa mkondo wa pili wa robo-fainali ya UEFA mnamo Aprili 19, 2023.

Mane alijiunga na Bayern kutoka Liverpool kwa ada ya Sh5.9 bilioni baada ya kutia saini mkataba wa miaka mitatu mnamo Juni 2022. Aliyoyomea Bayern kujaza pengo la mvamizi Robert Lewandowski aliyehamia Barcelona.

Alipachika kimiani mabao sita kutokana na mechi saba za kwanza katika mashindano yote yaliyonogeshwa na Bayern japo hajafunga goli lolote tangu Oktoba 2022.

Mane alifungia Liverpool mabao 120 kutokana na mechi 269 na alikosa kuchezea Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar kutokana na jeraha la goti alilolipata akiwajibikia Bayern mnamo Novemba 2022. Jeraha hilo lilimnyima pia uhondo wa kuchezea Bayern katika mechi tisa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri Mackenzie ajisalimisha kwa polisi manusura wa...

Mke wa Achraf Hakimi aliyeomba talaka akitaka afaidi mali...

T L