• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Braut Haaland si wa kuuzwa hivi karibuni – Borussia Dortmund

Braut Haaland si wa kuuzwa hivi karibuni – Borussia Dortmund

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund wamefutilia mbali uwezekano wa kumtia mnadani fowadi Erling Braut Haaland muhula huu licha ya sogora huyo raia wa Norway kuhemewa pakubwa na Chelsea.

Kocha Thomas Tuchel wa Chelsea ni miongoni mwa wakufunzi ambao wamekuwa wakimvizia sana Haaland aliyefungia Red Bull Salzburg ya Austria na Dortmund ya Ujerumani jumla ya mabao 20 kutokana na mechi 16 pekee za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mbali na Chelsea, kikosi kingine kinachowania maarifa ya Haaland ambaye atatimu umri wa miaka 21 mnamo Julai 21, 2021 ni Manchester City ya kocha Pep Guardiola.

Man-City wanamsaka fowadi atakayeziba pengo la Sergio Aguero aliyejiunga na Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2020-21 baada ya mkataba wake uwanjani Etihad kutamatika rasmi.

Iwapo watakosa kumsajili Haaland ambaye wakala wake ni Mino Raiola, Man-City wamefichua mpango wa kuwania huduma za nahodha wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Uingereza, Harry Kane.

Man-City tayari wamefutilia mbali tetesi zinazowahusisha na uwezekano wa kusajili Antoine Griezmann wa Barcelona au Robert Lewandowski wa Bayern Munich katika juhudi za kuziba pengo la Aguero.

Dortmund tayari wameagana na mwanasoka matata raia wa Uingereza, Jadon Sancho, 21, ambaye amesajiliwa na Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kwa mujibu wa kikosi hicho, kuondoka kwa Haaland pia kutawatikisa pakubwa kadri wanavyojiandaa kwa soka ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na UEFA mnamo 2021-22.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wanavoliboli ya ufukweni Kenya kutumia ndege ya Ethiopia...

Wakazi wa South Ngariama walalamikia hali mbovu ya barabara