• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 5:45 AM
Wanavoliboli ya ufukweni Kenya kutumia ndege ya Ethiopia Airlines kuenda Olimpiki, waonya wapinzani

Wanavoliboli ya ufukweni Kenya kutumia ndege ya Ethiopia Airlines kuenda Olimpiki, waonya wapinzani

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya voliboli ya ufukweni ya Kenya imetuma onyo kwa wapinzani wake wa Kundi D kwenye Olimpiki 2020 inapojiandaa kutumia ndege ya Ethiopian Airlines kuelekea jijini Tokyo, Japan hapo Julai 17.

Brackcides Agala kutoka klabu ya Kenya Prisons na Gaudencia Makokha wa klabu ya Kenya Pipeline watakabiliana na Claes/Sponcil (Amerika), Ana Patricia/Rebecca (Brazil) na Anastasija Kravcenoka/Tina Graudina (Latvia) katika mechi za makundi.

Katika mahojiano na kocha wao Sammy Mulinge, alisema, “Wapinzani wetu kutoka Brazil, Amerika na Latvia wana ujuzi mwingi katika voliboli ya ufukweni. Ni kweli hata katika viwango bora vya mchezo huu wanaorodheshwa juu sana. Hata hivyo, sisi pia tuna uwezo. Tunawaheshimu, lakini hatuwaogopi.”

Mulinge aliongeza kuwa wachezaji wake wako sawa na kushukuru Mungu kuwa hakuna aliye na jeraha. Timu haziruhusiwi kubadilisha mchezaji kwa hivyo jeraha lolote litabandua Kenya.

“Tunafurahi pia tulipimwa virusi vya corona Jumatano (Julai 14) na hakuna aliyepatikana navyo. Tumepimwa virusi hivyo tena leo (Julai 16) na tunatumai kuwa matokeo yatakuwa sawa kabla tufunge safari ya kuenda Tokyo,” alisema Mulinge ambaye pia ni kocha mkuu wa klabu ya voliboli ya wanaume ya KPA.

Agala na Makokha, alisema Mulinge, wanasubiri kwa hamu kubwa Olimpiki. Aliongeza, “Tulikuwa na kipindi chetu cha mwisho cha mazoezi mepesi ya uwanjani hapo Alhamisi.”

Mulinge pia alieleza Taifa Leo kuwa wamepata kuwaona wapinzani wao wakiwemo Wabrazil Patricia na Rebecca.

Dhidi ya Wabrazil hao, Mulinge amesema kuwa Wakenya watalazimika kutumia zaidi mbinu ya kuzuia makombora karibu na neti na pia kuwa na shabaha katika kuanzisha mipira kwa sababu “ni wazuri sana katika uzuiaji wa makombora”.

“Tunaenda kucheza katika kiwango tofauti kwa hivyo pia tumeandaa wachezaji wetu kiakili na hatutapuuza chochote,” alisema kabla ya kuongeza kuwa Kenya iko makini sana kukumbukwa kwa mazuri katika kampeni hiyo yake ya kwanza ya voliboli ya ufukweni kwenye Olimpiki.

“Tunalenga kupigania kupata alama na hata seti katika kila mechi. Tunajua kibarua ni kigumu na pia timu nyingi nje ya Afrika zinatuchukulia kuwa wanyonge, lakini tutajitahidi kuhakikisha kuwa kampeni yetu haitakuwa kutalii nchini Japan.”

Aidha, Mulinge alieleza kusikitishwa kuwa wachezaji Phoscah Kasisi na Yvonne Wavinya hawakuweza kujumuishwa katika timu ya taifa ya Kenya.

“Tumeelezwa kuwa Japan haitaki wageni wengi, hasa ambao hawatahusishwa moja kwa moja katika mashindano. Nasikitikia Kasisi na Wavinya kwa sababu walichangia pakubwa katika Kenya kushinda voliboli ya ufukweni ya Afrika mwezi Juni tukifuzu kushiriki Olimpiki. Wangetusaidia sana katika mazoezi kwa sababu kKufanya mazoezi bila mpinzani pia kuna changamoto zake. Hata hivyo, hatuna budi bali kukubali kuwa ni wachezaji wawili pekee wameruhusiwa kutoka mchezo huu nchini Kenya kushiriki Olimpiki,” alihitimisha.

  • Tags

You can share this post!

Babu, 93 ashinda vijana kwa mistari, aoa mke wa umri wa...

Braut Haaland si wa kuuzwa hivi karibuni – Borussia...