• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Burnley wamtimua kocha Sean Dyche

Burnley wamtimua kocha Sean Dyche

Na MASHIRIKA

BURNLEY wamemfuta kazi kocha Sean Dyche zikisalia mechi nane pekee kabla ya kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kutamatika rasmi.

Kikosi hicho ambacho kimepoteza mechi tano kati ya sita zilizopita katika EPL, kwa sasa kinashikilia nafasi ya 18 jedwalini baada ya kujizolea alama 24 kutokana na michuano 30. Ni pengo la pointi tatu pekee ambalo linatenganisha Burnley na Norwich City wanaovuta mkia baada ya mechi 31.

Hadi kutimuliwa kwake, Dyche ndiye alikuwa mkufunzi aliyesimamia michuano mingi zaidi ya EPL tangu apokezwe mikoba ya kikosi hicho mnamo Oktoba 2012.

“Yalikuwa maamuzi mgumu kumwachisha Dyche kazi uwanjani Turf Moor. Hata hivyo, tunahisi kwamba huu ndio wakati mwafaka kwa mabadiliko kufanyika,” akasema Mwenyekiti wa Burnley, Alan Pace.

Mchuano wa mwisho kwa Dyche kusimamia kambini mwa Burnley ni ule wa EPL uliowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Norwich.

Mbali na Dyche, wengine ambao wameagana rasmi na Burnley ni kocha msaidizi Steve Stone na mkufunzi wa makipa, Billy Mercer.

Mechi ijayo ya EPL itakayokutanisha Burnley na West Ham United mnamo Aprili 17, 2022 ugani London itasimamiwa na Mike Jackson ambaye ni kocha wa chipukizi wa U-23. Atashirikiana na mkufunzi wa makipa Connor King na nahodha wa kikosi hicho, Ben Mee.

“Mchakato wa kutafuta kocha mrithi wa Dyche umeanza na tangazo kuhusu hatua tutakazopiga zitatolewa hivi karibuni,” ikasema sehemu ya taarifa ya Burnley.

Dyche alitia saini mkataba wa miaka minne kambini mwa Burnley mnamo Septemba 2021 na kandarasi hiyo ilitarajiwa kukatika Septemba 2025.

Akidhibiti mikoba ya Burnley, Dyche aliongoza kikosi hicho kupanda ngazi kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship) hadi EPL mara mbili. Aidha, klabu hiyo ilikamilisha kampeni za EPL ndani ya orodha ya 10-bora jedwalini mara mbili.

Isitoshe, aliongoza Burnley kunogesha soka ya bara Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 51 mnamo 2018-19 baada ya kukamilisha kipute cha EPL katika nafasi ya saba mnamo 2017-18.

Burnley wameshinda mechi nne pekee kutokana na 30 zilizopita ligini msimu huu, hiyo ikiwa rekodi yao duni zaidi katika historia yao kwenye kivumbi hicho.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Shujaa kikaangoni ikilenga robo-fainali Vancouver 7s

Frankfurt kukutana na West Ham kwenye nusu-fainali ya...

T L