• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Chelsea kusajili Raheem Sterling kujaza pengo la Lukaku anayemezewa upya na Inter Milan

Chelsea kusajili Raheem Sterling kujaza pengo la Lukaku anayemezewa upya na Inter Milan

Na MASHIRIKA

CHELSEA wako radhi kuweka mezani kima cha Sh5.2 bilioni ili kushawishi Raheem Sterling kubanduka Manchester City na kutua ugani Stamford Bridge kujaza pengo la Romelu Lukaku anayewaniwa upya na Inter Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Hali na mustakabali wa Sterling uwanjani Etihad unasalia tete ikizingatiwa kwamba amesalia na miezi 12 pekee katika mkataba wake wa sasa na Man-City. Isitoshe, miamba hao wanaomdumisha kwa ujira wa Sh44 milioni kwa wiki, tayari wamejinasia huduma za mvamizi Erling Braut Haaland aliyeagana na Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa Sh7.6 bilioni.

Hata hivyo, kuondoka kwa Sterling ugani Etihad huenda kukavuruga mpango wa Arsenal wa kumsajili mchana-nyavu Gabriel Jesus kutoka Man-City ambao ni wafalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Arsenal wako tayari kutoa Sh7.4 bilioni ili kushawishi Jesus kuziba pengo la mshambuliaji Alexandre Lacazette aliyerejea Olympique Lyon ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu mwanzoni mwa mwezi huu.

Japo Sterling, 27, anahemewa pia na Real Madrid ya Uhispania, anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Chelsea kwa kuwa matamanio yake ni kusalia EPL na kuendelea kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Atakuwa sogora wa kwanza wa haiba kubwa kusajiliwa na kocha Thomas Tuchel chini ya mmiliki mpya wa Chelsea, Todd Boehly, ambaye ana kibarua kizito cha kudumisha Hakim Ziyech, Timo Werner na Christian Pulisic ugani Stamford Bridge kadri anavyofukuzia pia maarifa ya Ousmane Dembele, Nathan Ake na Jules Kounde kutoka Barcelona, Man-City na Sevilla mtawalia.

Sterling aliingia katika sajili rasmi ya Man-City mnamo Julai 2015 baada ya kuagana na Liverpool kwa Sh6.9 bilioni. Ada hiyo, wakati huo, ndiyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa mchezaji raia wa Uingereza katika soko la uhamisho wa wanasoka.

Mchango wake katika safu ya mbele ya Man-City ulisaidia kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kunyanyua taji la EPL mnamo 2017-18 na 2018-19. Kufikia sasa, nyota huyo wa zamani wa Queens Park Rangers (QPR) amefungia Man-City magoli 131 kutokana na mechi 339 huku akijivunia mabao 19 kutokana na michuano 77 akivalia jezi za timu ya taifa.

Alicheka na nyavu za wapinzani mara 13 kutokana na mechi 30 za ligi mnamo 2021-22 na kuongoza waajiri wake kuzoa taji la nne la EPL chini ya Guardiola. Amenyanyua pia Kombe la FA na mataji manne ya League Cup akichezea Man-City.

Makali yake yalidhihirika zaidi katika pambano la mwisho katika EPL mnamo 2021-22 ambapo alichangia bao la Ilkay Gundogan lililowezesha Man-City kutoka nyuma kwa magoli 2-0 na kupepeta Aston Villa 3-2 uwanjani Etihad.

Ingawa hivyo, Sterling alisalia benchi katika mikondo miwili ya nusu-fainali za UEFA iliyoshuhudia Man-City wakibanduliwa na Real Madrid ya Uhispania kwa jumla ya mabao 6-5.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Madhila ajifunza maana ya msemo ‘subira huvuta...

Jubilee Mlimani waomba Raila msamaha na kuahidi kumpigia...

T L