• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Jubilee Mlimani waomba Raila msamaha na kuahidi kumpigia debe

Jubilee Mlimani waomba Raila msamaha na kuahidi kumpigia debe

NA MWANGI MUIRURI

VIONGOZI wa Jubilee kutoka Ukanda wa Mlima Kenya wameahidi kumuuza kikamilifu mwaniaji wa Urais wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga katika eneo hilo, kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kumekuwa na madai kuwa wanasiasa kutoka eneo la Kati, wamekuwa wakimakinikia tu kampeni zao na kukosa kumpigia debe Bw Odinga, kutokana na dhana kuwa hauziki kisiasa miongoni mwa jamii ya GEMA.

Hata hivyo, viongozi wa Jubilee na vyama tanzu Mlima Kenya, sasa wanasema kuwa watamuuza Bw Odinga na hata kutumia picha yake kwenye mabango yao ya kampeni.

Vilevile, Jubilee na vyama tanzu sasa vinashauriana kuhusu kuwasilisha mwaniaji mmoja katika kila nyadhifa ili kupambana na wale wa UDA ambayo inaoongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Hata hivyo, mpango huo umepingwa na vyama vidogo vinavyohisi vitalazimishwa kuwaunga mkono wagombeaji wa Jubilee pekee.

Bw Odinga anaonekana ameanza kupenya kisiasa katika eneo la Mlima Kenya hasa baada ya kumteua Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kama mgombeaji mwenza wake mwezi uliopita.

Mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth, katika mkutano aliohudhuria Bw Odinga eneo la Murang’a wiki jana, alisema kuwa upande wa UDA umekuwa ukiendeleza dhana kuwa waziri huyo mkuu wa zamani hawezi kupenya Mlima Kenya, ila ukweli ni kwamba wakazi watampigia kura Bw Odinga kwa wingi baada ya kutathmini na kugundua kuwa ndiye kiongozi anayefaa.

“Watu wetu walihadaiwa kuwa Raila ni adui wa Mlima Kenya na hawezi kupata kura hapa. Hata hivyo, mkondo wa sasa wa kisiasa unaonyesha kuwa yeye ndiye mwokozi wetu,” akasema Bw Kenneth.

Mbunge huyo wa zamani wa Gatanga, alisema kuwa umaarufu ambao Dkt Ruto amekuwa nao Mlima Kenya tangu 2013, unaendelea kutokomea akidai kuwa wakazi wengi wa Mlima Kenya washaanza kuhamia mrengo wa Azimio la Umoja.

Mwaniaji wa Ugavana wa Murang’a kupitia Jubilee, Bw Jamleck Kamau, alisema enzi za kujificha na kutomfanyia Bw Odinga kampeni zimepitwa na wakati na sasa wapo tayari kujihusisha na siasa zake hadharani.

“Tunaomba msamaha kuwa tumekuwa vuguvugu katika hatua ya kukuunga mkono. Hata hivyo, sasa mambo yametengenea na tutakuvumisha kila pembe ya Mlima Kenya bila kuhofia kupoteza kura,” akasema Bw Kamau, mbunge wa zamani wa Kigumo.

Aliongeza kuwa umaarufu wa UDA katika eneo hilo ndio uliwasababisha wawe na uungwaji mkono vuguvugu lakini sasa wapo tayari kurindima ngoma ya ‘baba’.

Kauli yake iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Jubilee katika Kaunti ya Kirinyaga Muriithi Kang’ara alisema kuwa umaarufu wa UDA na muungano wa Kenya Kwanza umepungua sana Mlima Kenya tangu Bw Odinga aanzishe kampeni kali eneo hilo na uteuzi wa Bi Karua.

“Mwanzoni upande wa Kenya Kwanza ndio ulikuwa na uungwaji mkono mkubwa sana hapa Mlima Kenya. Hata hivyo, kufikia Mei, Azimio imepiga hatua kubwa na sasa hatuna uoga tena tunapomfanyia Bw Odinga kampeni,” akasema Bw King’ara.

Alikariri kuwa kuchaguliwa kwa Bi Karua kama mgombeaji mwenza wa Bw Odinga kumempa umaarufu sana waziri huyo mkuu wa zamani Mlima Kenya na akaonyesha imani kuwa jamii ya Gema itamuunga mkono Bw Odinga.

Hata hivyo, mizozo ya mara kwa mara miongoni mwa vyama vilivyoko ndani ya Muungano wa Azimio la Umoja, huenda vikaathiri kampeni za Bw Odinga.

Baadhi ya vyama hivyo vinalalamika kuwa wawaniaji wao wanashurutishwa watupilie mbali azma yao na kumuunga mkono wawaniaji wa Jubilee.

Aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Elimu Zack Kinuthia ambaye analenga kiti cha ubunge Kigumo, anadai kuwa amekuwa akishawishiwa na baadhi ya wanasiasa wakuu atupilie mbali azma yake, na amuunge mkono mbunge wa sasa Mwaniki Wangari wa Jubilee.

Bw Kinuthia anawania kiti hicho kupitia PNU anayoingoza Waziri wa Kilimo Peter Munya.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea kusajili Raheem Sterling kujaza pengo la Lukaku...

Babu Owino akana madai kwamba alichochea fujo Jacaranda

T L