• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Chelsea wasubiri hadi dakika za mwisho kubandua Brentford kwenye Carabao Cup

Chelsea wasubiri hadi dakika za mwisho kubandua Brentford kwenye Carabao Cup

Na MASHIRIKA

CHELSEA walitinga nusu-fainali ya tatu ya mashindano ya haiba katika kipindi cha miezi 11 chini ya kocha Thomas Tuchel baada ya kufunga mabao mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwabandua majirani zao Brentford kwenye robo-fainali za Carabao Cup.

Beki Pontus Jansson alijifunga katika dakika ya 80 kabla ya Jorginho kuwapachikia Chelsea goli la pili kupitia penalti dakika tano baadaye. Ushindi huo uliwapa Chelsea fursa ya kutinga nusu-fainali za Carabao Cup kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu na sasa watavaana na Tottenham Hotspur katika hatua ya nne-bora.

Baada ya corona na majeraha kuvuruga uteuzi wake wa kikosi cha kwanza, Tuchel aliwajibisha matineja watatu kwa mara ya kwanza akiwemo Harvey Vale, 18, aliyepoteza nafasi ya wazi ya kuwaweka Chelsea kifua mbele katika kipindi cha kwanza. Brentford walianza mchezo huo kwa matao ya juu huku wakimwajibisha vilivyo kipa Kepa Arrizabalaga aliyelazimika kupangua fataki kali alizoelekezewa na Yoane Wissa, Mathias Jensen na Rico Henry.

Jansson alijifunga katika dakika ya 80 baada ya kushindwa kudhibiti krosi ya Reece James. Jorginho alifanya mambo kuwa 2-0 dakika tano baadaye kupitia penalti iliyookana na hatua ya Alvaro Fernandez kumchezea visivyo Christian Pulisic ndani ya kijisanduku.

Chelsea waliingia ugani wakiwa na kiu ya kusajili matokeo ya kuridhisha baada ya kushinda mechi moja pekee kati ya tano za awali. Mbali na Vale, chipukizi wengine waliotegemewa na Chelsea dhidi ya Brentford ni Jude Soonsup-Bell, 17, na Xavier Simons, 18, ambaye ni mchezaji wa zamani wa akademia ya Brentford.

Soonsup-Bell alikuwa na miaka minane pekee wakati beki Cesar Azpilicueta alipokuwa akiwajibishwa na Chelsea kwa mara ya kwanza mnamo 2012. Chelsea walileta uwanjani masogora tegemeo Jorginho, James, Pulisic, Mason Mount na N’Golo Kante katika kipindi cha pili baada ya dakika 79 za kwanza kukamilika kwa sare tasa.

Brentford waliotinga nusu-fainali za Carabao Cup mnamo 2020-21, sasa wataelekeza mawazo zaidi kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambapo wanashikilia nafasi ya 12 kwa alama 20 sawa na Crystal Palace na Brighton.

You can share this post!

Spurs yakung’uta West Ham na kutinga nne-bora Carabao...

Liverpool wadengua Leicester kwenye robo-fainali za Carabao...

T L