• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Chelsea pua na mdomo kuingia 16-bora UEFA baada ya kutandika Malmo ugenini

Chelsea pua na mdomo kuingia 16-bora UEFA baada ya kutandika Malmo ugenini

Na MASHIRIKA

CHELSEA sasa wako pua na mdomo kuingia hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kucharaza Malmo ya Uswidi 1-0 mnamo Jumanne usiku ugenini.

Bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo lilifumwa wavuni na Hakim Ziyech baada ya kushirikiana vilivyo na Callum Hudson-Odoi katika dakika ya 56.

Nusura Thiago Silva afungie Chelsea bao la pili katika kipindi cha pili ila mpira aliouelekeza langoni kwa kichwa ukaondolewa na Anel Ahmedhodzic wa Malmo kwenye mstari wa goli. Mabeki wa Chelsea walisalia imara na kuwanyima Malmo fursa ya kuelekeza kombora lolote lililolenga shabaha langoni mwao.

Kufikia sasa, Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wa UEFA, wanashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi H kwa alama tisa kutokana na mechi nne. Ni pengo la pointi tatu ndilo linatamalaki kati yao na viongozi Juventus ambao tayari wamefuzu kwa hatua ya mwondoano baada ya kupepeta Zenit St Petersburg 4-2 mnamo Jumanne usiku jijini Turin, Italia.

Chini ya kocha Thomas Tuchel, Chelsea sasa wanahitaji alama moja pekee kutokana na mechi mbili zijazo za Kundi H dhidi ya Juventus na Zenit ili kuingia hatua ya 16-bora ya UEFA muhula huu.

Wakinolewa na mvamizi wa zamani wa Newcastle United, Jon Dahl Tomasson, Malmo walikuwa wakisakata mchuano wao wa 12 wa UEFA msimu huu baada ya kunogesha raundi nne za kufuzu na kudengua Rangers ya Scotland katika safari ya kuingia hatua ya makundi.

Chelsea walipepetana na Malmo katika mchuano huo bila kujivunia huduma za mafowadi wao tegemeo – Romelu Lukaku na Timo Werner wanaouguza majeraha na Mason Mount anayeugua.

Mechi hiyo ilitoa fursa kwa Chelsea kumwajibisha mshambuliaji raia wa Amerika, Christian Pulisic kwa mara ya kwanza tangu jeraha la goti limweke mkekani kwa miezi miwili kuanzia Agosti 2021.

Ilikuwa mechi ya 10 kutokana na 17 za mapambano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu kwa Chelsea kusakata bila ya kufungwa bao.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ronaldo aokoa Manchester United kinywani mwa Atalanta...

Juventus wakomoa Zenit na kuingia 16-bora UEFA

T L