• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Ronaldo aokoa Manchester United kinywani mwa Atalanta katika soka ya bara Ulaya nchini Italia

Ronaldo aokoa Manchester United kinywani mwa Atalanta katika soka ya bara Ulaya nchini Italia

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alibeba Manchester United kwa mara nyingine baada ya kufunga bao la dakika za mwisho lililowawezesha kusajili sare muhimu ya 2-2 dhidi ya Atalanta katika mechi ya Kundi F ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku nchini Italia.

Ronaldo, 36, alirejesha Man-United mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kufuta juhudi za Josip Ilicic aliyewaweka Atalanta kifua mbele katika dakika ya 12 uwanjani Gewiss, Bergamo. Hata hivyo, Atalanta walidhani walikuwa wameshinda mechi hiyo baada ya Duvan Zapata kuwafungia bao la pili katika dakika ya 56.

Ronaldo alishirikiana na Bruno Fernandes mwishoni mwa kipindi cha pili na kumwacha hoi kipa Juan Musso wa Atalanta na hivyo kuvunia waajiri wake alama moja iliyowadumisha kileleni mwa Kundi F kwa alama saba.

Atalanta sasa wanajivunia alama tano zinazowaweka katika nafasi ya tatu nyuma ya Villarreal ambao pia wamejizolea pointi saba kutokana na mechi nne zilizopita za Kundi F.

Ronaldo alirejea ugani Old Trafford mwanzoni mwa msimu huu kuvalia tena jezi za Man-United baada ya kuagana na Juventus ya Italia. Nyota huyo raia wa Ureno amewahi pia kuchezea Real Madrid ya Uhispania. Sasa amefunga bao katika kila mojawapo ya mechi za Man-United katika hatua ya makundi ya UEFA muhula huu.

Man-United walijibwaga ugani kwa ajili ya mechi hiyo siku tatu baada ya kuwazamisha Tottenham Hotspur 3-0 kwenye gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Ilikuwa mara ya tisa kutokana na mechi 14 zilizopita chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa Man-United kufungwa kwanza katika soka ya UEFA. Pigo la pekee kwa Man-United ni jeraha ambalo sasa huenda likamweka nje beki Raphael Varane wakati wa mechi ya EPL itakayokutanisha waajiri wake na Manchester City mnamo Novemba 6 ugani Old Trafford.

Bao la pili la Ronaldo dhidi ya Atalanta lilikuwa lake la 127 akivalia jezi za Man-United katika mapambano yote. Mbali na kuvunja rekodi ya ufungaji iliyowekwa na Solskjaer aliyechezea Man-United kati ya 1996 na 2007, Ronaldo alimpunguzia mkufunzi wake huyo presha tele ya kutimuliwa tangu Man-United wapepetwe 5-0 na Liverpool kwenye gozi la EPL mnamo Oktoba 24, 2021 ugani Old Trafford.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uhuru ahimiza viongozi kukabili mabadiliko ya tabianchi

Chelsea pua na mdomo kuingia 16-bora UEFA baada ya...

T L