• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
COVID-19: Tuzo za washindi wa Kombe la FA zapunguzwa kwa asilimia 50

COVID-19: Tuzo za washindi wa Kombe la FA zapunguzwa kwa asilimia 50

Na MASHIRIKA

WAFALME wa Kombe la FA msimu huu wa 2020-21 watatia mfukoni Sh476 milioni pekee, hii ikiwa nusu ya kiasi cha fedha kilichotolewa kwa Arsenal waliotawazwa mabingwa wa taji hilo msimu uliopita wa 2019-20.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal almaarufu The Gunners waliwalaza Chelsea 2-1 kwenye fainali iliyochezewa uwanjani Wembley mnamo Mei 2020 na kujizolea jumla ya Sh952 milioni.

Arsenal walituzwa pia kima cha Sh504 milioni kwa kuibuka washindi wa hatua zote nyinginezo kabla ya kutinga fainali.

Lakini mwaka huu, Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) limepunguza tuzo ambazo washindi wa taji hilo watajizolea kwa asilimia 50.

Kutokuwepo kwa mashabiki uwanjani katika sehemu kubwa ya kampeni za kivumbi hicho kunamaanisha kwamba waandalizi wamefungiwa njia nyinginezo za fedha ambazo zingetolewa kwa washindi.

Kombe la FA ndilo shindano kongwe zaidi miongoni mwa mapambano yote mengineyo ya soka duniani.

Kinyume na hali ilivyokuwa msimu uliopita, washindi wa hatua ya raundi ya tatu muhula huu watatuzwa Sh8.6 milioni pekee. Washindi wa hatua hiyo msimu uliopita walitia kapuni Sh18.9 milioni kila mmoja.

Vikosi vitakavyobanduliwa kwenye hatua hiyo ya raundi ya tatu ama kwa kushindwa au kulemewa kucheza kutokana na janga la corona vitajizolea jumla ya Sh2.8 milioni kila kimoja.

Washindi wa mechi za raundi ya nne watatuzwa Sh12.6 milioni kila mmoja huku watakaotinga raundi ya tano wakijizolea Sh25.2 milioni kila mmoja.

Timu zitakazofuzu kwa hatua ya robo-fainali zitajizolea Sh50.4 milioni kila mmoja huku Sh126 milioni zikiendea kila mshindi wa mechi za hatua ya nusu-fainali.

Vikosi vitakavyoondolewa kwenye hatua ya nusu-fainali vitapokezwa kima cha Sh63 milioni kila kimoja huku kila mojawapo ya timu zitakazosonga mbele hadi fainali ikituzwa Sh252 milioni za ziada.

Chelsea walituzwa Sh252 milioni mnamo 2019-20 kwa kuzidiwa ujanja na Arsenal kwenye fainali ya msimu uliopita. Fedha hizo zimepunguzwa kwa asilimia 50 msimu huu. Hivyo, atakayepoteza fainali atapokezwa kima cha Sh126 milioni pekee.

Fedha ambazo washiriki wa Kombe la FA walikuwa wakipokezwa katika kila hatua ziliongezwa maradufu mwanzoni mwa msimu wa 2018-19 kwa nia ya kuhimiza vikosi kuchukulia kampeni za kuwania ubingwa wa taji hilo kwa uzingativu zaidi.

You can share this post!

Leicester kukosa huduma za Vardy na Maddison kwenye mechi...

Wolves wang’ata Palace na kufuzu kwa raundi ya nne ya...