• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
DOUGLAS MUTUA: Wakenya watumie akili kabla ya mambo kuharibika

DOUGLAS MUTUA: Wakenya watumie akili kabla ya mambo kuharibika

Na DOUGLAS MUTUA

HIVI Kenya hiki ni kitu gani ambacho kinaendelea kama kinavyostahili siku hizi? Orodhesha: michezo, siasa, uchumi. Hamna! Tunachekwa na kila mtu.

Inawezekanaje Waganda wanatushinda mbio na, kana kwamba ushinde wenyewe hautoshi, wanakimbia mitandaoni kutuonya tusidai wanariadha wao bora ni wetu?

Kwenye siasa tumezembea, tunawasubiri wakongwe wa upinzani waliojiingiza serikalini watoke huko waje kutukomboa kutoka minyororo ya ukoloni mambo-leo.

Kiuchumi, kukosa pesa imekuwa desturi, kuwa nazo ni ajabu au muujiza nadra sana kutokea, lakini tunakubali hiyo ndiyo hali yetu na tunaishi nayo.

Maisha yanazidi kuwa magumu nchini Kenya, taifa lenye watu waliojaa kiburi kiasi cha kudai Mungu anawapenda kwa sababu halina vita kama mataifa jirani.

Ungedhani Mungu anaichukia Somalia, Sudan Kusini, Uganda, Ethiopia na mataifa mengine yenye misukosuko ya kisiasa.

Binafsi ni natamani sana kila kitu kiharibike kiasi cha watu kukosa sashi ya kwendea haja ili angaa akili zetu zembe zigutuke na kuanza kufanya kazi. Zimelala usingizi wa pono.

Tumekuwa wazembe hivi kwamba hata mambo yanapoendelea vibaya hakuna mashujaa wa kujitolea ama kutafuta suluhu au kupinga utawala mbovu.

Ona sasa aibu ambayo tumejizolea kwenye michezo ya Olimpiki nchini Japan! Michezo tuliyozoea kushinda tangu hapo imekuwa himaya ya watu tuliowadhani wazembe.

Hadi wakati wa kuiandika makala hii, timu ya Kenya ya Olimpiki ilikuwa imepata nishani ya dhahabu moja pekee hali mbio zetu za kawaida zilikwisha kamilika na tukashindwa.

Mbio za mita 10,000, 5,000 na hata 3,000 kuruka vizuizi na maji zilikwisha shindwa na watu, tukaondoka viwanjani huku nyuso kainama kwa fedheha, utadhani tunataka kusujudu.

Maandalizi ya michezo hiyo yalikuwa duni, ndiposa mashujaa kama Hellen Obiri wakaponyokwa na dhahabu, lakini bado hatutafanya chochote kurekebisha makosa yetu.

Visingizio vitatolewa, wasimamizi wa michezo waliochemsha waachwe walipo penye vyeo vyao, kufumba na kufumbua olimpiki ijayo ifike, tushindwe kama kawaida.

Nasisitiza kwamba ni heri mambo yaharibike ili tutie akili kuhusu siasa, uchumi na jamii. Niliandika hayo Bw Raila Odinga aliporidhiana na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018.

Wakati huo nilisema labda Bw Odinga alikuwa amechoshwa na Wakenya waliodai kuwa watetezi wa demokrasia kwa kumtegemea katika siasa za mapambano. Kila mtu ana haki ya kupumzika na kuishi kwa amani uzeeni.

Tazama nchi ilivyo sasa, imepooza kisiasa tangu wakati huo. Kila wakati watawala wetu wakifanya ya hovyo tunakereka ndani kwa ndani, hatujasirii kumwagika barabarani.

Nakuhakikishia Bw Odinga angekuwa upinzani kisha aseme tujitokeze, tungefanya hivyo kwa fujo. Hii ni tabia ya kipumbavu inayostahili kulaaniwa.

Kwani sisi hatujui shida zetu? Na kama tunazijua, kwani hazituumi kiasi cha kuzitafutia sulu kivyetu? Lazima tumsubiri Bw Odinga? Namwomba afurahie maisha huko aliko.

Yetu ikmekuwa serikali ya kukopa, kupora na kutuachia madeni ya Wachina ambayo tutalipa vizazi baada ya vizazi. Tayari umaskini unatuchoma kama mkuki!

Michango ya kupambana na korona ilishuka nchini kwa mabilioni, ikaibwa karibu yote, tukafungiwa biashara na njia zote za kujiruzuku, lakini hatufanyi chochote.

Hatujali, tunapiga nyoyo konde na kujiambia Mungu anatupenda kuliko majirani zetu kweli ikiwa tungali hai.

Ajenda Nne za maendeleo tulizoahidiwa na utawala wa sasa ndio zimeanza kuchangishiwa fedha Uingereza ili zifufuliwe, mwaka mmoja kabla ya mtu kustaafu. Na tunaona ni kitu kizuri sana ati, tunashangilia.

Mtesi wetu tunamjua, wala hatuchukui hatua yoyote ila kumshukuru Mungu kwa kutuweka hai. Labda tunasubiri muujiza. Huo ni uzembe. Hatutapata muujiza wowote.

Kenya itabadilika kuwa taifa la kupigiwa mfano ikiwa kila mtu atajituma kurekebisha mambo, tuache ukabila, kiburi na uzembe. Na zaidi tuvipende vitabu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Uthiru Vision tumepania kushriki ligi kuu Kenya lakini...

WANDERI KAMAU: Tubuni makavazi ya uanahabari kukuza...