• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Eliud Kipchoge alenga kufanya kitu atakachokumbukwa nacho kwa muda mrefu kwenye Olimpiki

Eliud Kipchoge alenga kufanya kitu atakachokumbukwa nacho kwa muda mrefu kwenye Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mtetezi Eliud Kipchoge ametangaza kuwa misheni yake kubwa si kushiriki tu marathon kwenye Olimpiki 2020, bali kuweka historia nyingine.

Kipchoge ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya wanaume ya saa 2:01:39 aliyoweka kwenye Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2018.

Pia, Kipchoge, 36, ndiye mtu wa kwanza duniani kukamilisha umbali huo chini ya saa mbili baada ya kutimka mbio maalum za INEOS1:59 kwa saa 1:59:40 jijini Vienna, Austria mwaka 2019.

Tangu michezo ya Olimpiki ianzishwe mwaka 1896, ni wanaume wawili pekee duniani wamefanikiwa kutetea taji lao la mbio za kilomita 42. Muethiopia Abeba Bikila alizoa taji la mwaka 1960 jijini Roma, Italia kabla ya kulitetea miaka minne baadaye jijini Tokyo, Japan.

Mjerumani Waldemar Cierpinski aliibuka bingwa mwaka 1976 jijini Montreal, Canada na 1980 jijini Moscow, Urusi.

Katika mahojiano na timu yake ya NN Marathon, Kipchoge, ambaye anafahamika kwa jina la utani kama “The Philosopher”, alisema, “Kitakachonichochea zaidi jijini Tokyo si shiriki michezo ya Olimpiki, ni kufanya kitu ambacho nitakumbukwa nacho kwa muda mrefu.”

Kipchoge ni Mkenya wa pili mwanamume kutwaa taji la marathon la Olimpiki baada ya Samuel Wanjiru mwaka 2008 jijini Beijing, Uchina. Alinyakua taji la Olimpiki za Rio de Janeiro nchini Brazil mwaka 2016.

Yeye ni mmoja wa wanamichezo ambao Kenya ina matumaini makubwa kupata medali kutoka kwao. Kipchoge atatimka Agosti 8 ambayo ni siku ya mwisho ya Olimpiki za Tokyo zitakazoanza Julai 23. Kuna uwezekano mkubwa hii itakuwa mara yake ya mwisho kushiriki Olimpiki kwa sababu atakuwa na umri wa miaka 39 wakati wa makala yajayo yatakayofanyika jijini Paris, Ufaransa mwaka 2024.

Kikosi cha marathon cha Kenya kitaelekea Tokyo mnamo Agosti 2. Mbali na Kipchoge, Kenya pia itawakilishwa katika marathon jijini Sapporo na Amos Kipruto, Lawrence Cherono, dunia wa dunia Ruth Chepng’etich na washikilizi wa rekodi ya dunia kilomita 21 Peres Jepchirchir na kilomita 42 Brigid Kosgei.

Kipchoge amekiri kuwa anatarajia ushindani mkali kwenye Olimpiki anapolenga kufuata nyayo za Bikila. Timu ya Kenya ya marathon inanolewa na makocha Patrick Sang na Eric Kimaiyo.

You can share this post!

KAMAU: Waraka wa wazi kwa wenyeji wa Kiambaa

AKILIMALI: Ndege wa mapambo wanavyompa tonge nono mwalimu...