• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Eliud Kipchoge azoa taji lake la tano la Berlin Marathon

Eliud Kipchoge azoa taji lake la tano la Berlin Marathon

NA GEOFFREY ANENE

BINGWA Eliud Kipchoge ameonyesha weledi wake katika mbio za kilomita 42 baada ya kushinda taji lake la tano la Berlin Marathon nchini Ujerumani, Jumapili.

Bingwa huyo alishinda marathon hiyo yake ya 16 kati ya 19 ameshiriki kwa saa 2:02:42 akifuta rekodi ya dunia ya 2:01:09 aliweka akishinda jijini Berlin mwaka 2022.

Kipchoge, ambaye anapanga kushiriki Olimpiki jijini Paris nchini Ufaransa mwaka 2024, alisalia mbele pekee yake baada ya kilomita ya 32 kufuatia Muethiopia Derseh Kindie,24, kusalimu amri.

Mtimkaji huyo atakayegonga umri wa miaka 39 hapo Novemba 5, alikuwa bega kwa bega na Kindie kutoka mwanzo na hata Kindie alichukua uongozi mara tatu kabla ya kubanduka.

Kipchoge alifuatiwa kwa karibu na Vincent Kipkemoi (2:03:13) na Muethiopia Tadese Takele (2:03:24).

Bingwa wa London Marathon Amos Kipruto aliyekuwa amepigiwa upatu kusumbua Kipchoge alififia baada ya kutupa nafasi ya pili akimaliza nambari saba 02:04:49.

Nafasi tatu za kwanza zilituzwa Sh7.2 milioni, Sh3.7m na Sh1.8m, mtawalia.

Makala haya ya 49 yalivutia jumla ya washiriki 60,000 wakiwemo wakiambiaji 47,912 kutoka mataifa 156 na waendeshaji 95 wa baiskeli ya kutumia mikono na karibu watoto 8,500.

Kundi la kupigania masuala ya tabianchi la “Last Generation” lilitarajiwa kutumia fursa ya mashindano hayo makubwa kuandamana.

Taarifa nchini Ujerumani zilisema kuwa maafisa 500 wa polisi walishika doria Jumamosi na wengine 650 Jumapili kuelekeza magari na kuweka usalama.

Mataji mengine Kipchoge anajivunia katika Marathon Kuu Duniani (WMM) ni Chicago Marathon (2014), London Marathon (2015, 2016, 2018 & 2019) na Tokyo Marathon (2022).

Bingwa huyo wa Olimpiki mwaka 2016 na 2021 hajashiriki New York City Marathon pekee katika ligi hiyo ya WMM inayofanyika katika miji ya Tokyo, Boston, London, Berlin, Chicago na New York.

Aliingia Berlin Marathon baada ya kusikitisha katika nafasi ya sita mjini Boston mnamo Aprili 17, 2023.

Mkenya Sheila Chepkirui ameridhika na nafasi ya pili katika kitengo cha akina dada kwa dakika 2:17:49 baada ya Muethiopia Tigist Assefa kuhifadhi taji kwa rekodi mpya ya dunia ya 2:11:52. Assefa amefuta rekodi ya Mkenya Brigid Kosgei ya 2:14:04 iliyowekwa kwenye Chicago Marathon mwaka 2019.

  • Tags

You can share this post!

Wa Iria ‘amshambulia’ Gavana Kahiga kwa kumfinyia jicho

Huzuni baba akiua mwanawe Narok kwa kumkatakata kwa kisu  

T L