• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 11:13 AM
Everton waomba Ubelgiji wamruhusu Roberto Martinez awe kocha wao mpya

Everton waomba Ubelgiji wamruhusu Roberto Martinez awe kocha wao mpya

Na MASHIRIKA

EVERTON wamemzungumzia kocha wao wa zamani, Roberto Martinez kuhusu uwezekano wa kurejea ugani Goodison Park kudhibiti mikoba ya kikosi hicho.

Kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kimewasiliana pia na Shirikisho la Soka la Ubelgiji (BFA) kuhusu uwezekano wa kuachilia Martinez kujiunga nao ili kujaza pengo la mkufunzi Rafael Benitez aliyefutwa kazi mnamo Januari 16, 2022 kutokana na msururu wa matokeo duni.

Hata hivyo, Ubelgiji wanaoorodheshwa wa kwanza kimataifa kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), wameshikilia kwamba hawako radhi kumwachilia kocha huyo raia wa Uhispania.

Martinez, 48, kwa sasa anakiandaa kikosi chake kwa ajili ya fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar kati ya Novemba na Disemba 2022. Ubelgiji ni miongoni mwa vikosi vinavyopigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa kivumbi hicho.

Martinez aliwahi kudhibiti mikoba ya Everton kuanzia 2013 hadi alipotimuliwa mnamo 2016. Aliajiriwa kuwa kocha wa Ubelgiji mnamo Agosti 2016.

Martinez angali anajivunia uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wasimamizi wa Everton licha ya kuwa mkufunzi wa kwanza kati ya watano kuwahi kutimuliwa na kikosi hicho chini ya mmiliki Farhad Moshiri. Martinez alifutwa kazi na Everton mnamo Mei 2016 baada ya kudhibiti mikoba ya kikosi hicho kwa misimu mitatu.

Mbali na Martinez, wakufunzi wengine wanaopigiwa upatu kutwaa mikoba ya Everton ni Wayne Rooney, Frank Lampard, Duncan Ferguson na Graham Potter.

You can share this post!

Bawabu ashtakiwa kuua mke aliyemweleza ameshindwa kitandani

AFCON: Tunisia waponda Mauritania bila huruma katika Kundi F

T L