• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Benitez katika presha ya kupigwa kalamu baada ya Everton kupepetwa na Palace ligini

Benitez katika presha ya kupigwa kalamu baada ya Everton kupepetwa na Palace ligini

Na MASHIRIKA

PANDASHUKA za Everton ugani msimu huu ziliendelezwa na Crystal Palace kwa kichapo cha 3-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Selhurst Park.

Kocha Rafael Benitez alizomea na mashabiki wakati wa mechi hiyo kutokana na hatua yake ya kuondoa ugani mvamizi Richarlson Andrade wa Brazil.

Pasi ya Demarai Gray aliyeshirikiana na Jordan Ayew ilichangia bao la kwanza ambalo Everton walifungiwa na Conor Gallagher mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Goli hilo lilikuwa la tano kwa Gallagher kufunga ligini msimu huu tangu ajiunge na Leicester kutoka Chelsea kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu.

Matokeo yakiwa 1-0, Benitez aliondoa Richarlson na nafasi yake kutwaliwa na Salomon Rondon. James Tomkins alifanya mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 62. Bao hilo lilichangiwa na Will Hughes aliyekuwa akichezea Palace kwa mara ya kwanza tangu Agosti.

Ingawa Rondon aliyefunga bao la kwanza ndani ya jezi za Everton alirejesha waajiri wake mchezoni katika dakika ya 70, Palace walipata bao la tatu kupitia Gallagher mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kichapo kutoka kwa Palace kinamaanisha kwamba Everton kwa sasa wamepoteza mechi nne kutokana na tano zilizopita. Matokeo hayo yanaweka Benitez katika hatari ya kupigwa kalamu iwapo watashindwa kutamba dhidi ya Chelsea ligini mnamo Disemba 16, 2021 ugani Stamford Bridge.

Palace kwa upande wao watakuwa wenyeji wa Southampton ugani Selhurst Park mnamo Disemba 15, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Polisi watano wapinga tuhuma katika kesi ambapo mahabusu...

Leicester City yajinyanyua na kunyanyasa Newcastle katika...

T L