• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Leicester City yajinyanyua na kunyanyasa Newcastle katika EPL

Leicester City yajinyanyua na kunyanyasa Newcastle katika EPL

Na MASHIRIKA

YOURI Tielemans alifunga mabao mawili na kusaidia waajiri wake Leicester City kujinyanyua baada ya maruerue ya kubanduliwa kwenye Europa League na kutandika Newcastle United 4-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani King Power.

Akicheza ligini kwa mara ya kwanza tangu Novemba 7, 2021 baada ya kuwekwa nje na jeraha la mguu, Tielemans alifunga penalti katika dakika ya 38. Hiyo ilikuwa baada ya Jamaal Lascelles kumkabili visivyo James Maddison ndani ya kijisanduku.

Ushirikiano mkubwa kati ya Maddison na Harvey Barnes ulichangia bao la pili ambalo Leicester walifungiwa na Patson Daka katika dakika ya 57. Tielemans alifungia Leicester goli la tatu kunako dakika ya 81, nne kabla ya Maddison kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao.

Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester walishuka dimbani siku tatu baada ya kudenguliwa na Napoli kwenye Europa League kwa kichapo cha 3-2.

Ushindi wao dhidi ya Newcastle ulikuwa wa pili baada ya mechi saba ligini. Matokeo hayo yaliwapaisha hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 22, sita nyuma ya West Ham United wanaofunga orodha ya nne-bora.

Newcastle kwa upande wao walisalia katika nafasi ya 19 kwa alama 10 sawa na Norwich City wanaovuta mkia. Masogora hao wa kocha Eddie Howe sasa wanakabiliwa na kibarua kizito dhidi ya Liverpool, Manchester City na Manchester United kwa usanjari huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Benitez katika presha ya kupigwa kalamu baada ya Everton...

Wafichua ukatili wa genge la askari jijini

T L