• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Fahamu tano bora za KWPL

Fahamu tano bora za KWPL

NA AREGE RUTH 

HUKU timu zikiendelea kujiandaa kwa raundi ya saba ya michuano ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) wikendi hii, kumeshuhudiwa ushindani mkali msimu huu wa 2022/23 ikilinganishwa na msimu jana.

Msimu jana chini ya Kamati ya Mpito, mabingwa mara tatu KWPL Vihiga Queens walitwaa ubingwa wa ligi. Baadae msimu huo ulitupiliwa mbali na Kamati ya Kitaifa (NEC) ya Shirikisho la Soka nchini (FKF). Kwa sasa Thika Queens ndio mabingwa watetezi.

Vihiga ambao bado hawajapoteza mechi yoyote kufikia sasa, wanakaa kileleni mwa jedwali wakiwa na alama 16. Wamevuna ushindi mara sita na kupata sare moja.

Wachezaji wanne wa timu hiyo, wanaongoza kwenye jedwali la wafungaji bora. Mshambuliaji Maureen Ater ana mabao matano, kiungo Mary Moraa Bundi amecheka na wavu mara nne nao Faith Ongachi na Yvonne Kaver wamefunga mabao mawili kila mmoja.

Katika nafasi ya pili, Nakuru City Queens hawashikiki msimu huu. Waliwaangusha mabingwa watetezi Thika kwa kuwapiga 2-1 nyumbani kwao ugani Thika. Wikendi iliyopita waliwanyeshea Ulinzi Starlets 3-1 uwanjani Ulinzi Sports Complex.

Baada ya mechi hiyo, walipanda hadi nafasi ya pili wakiwa na alama 13, alama tatu nyuma ya Vihiga. Wameshinda mechi nne wakapiga sare moja na kupoteza mechi moja.

Wafungaji bora kwenye timu hiyo ni Elizabeth Muteshi na mabao manne, Melon Mulindi akiwa na mabao matatu na Ruth Chebungei ambaye ana mabao mawili.

Zetech Sparks na Ulinzi wanafuata katika nafasi ya tatu na nne mtawalia kwenye jedwali wakiwa na alama kumi kila mmoja.

Timu hizi zinaaminika kuwa ni watani wajadi na wote huwa wanatoshana nguvu wanapokutana. Kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi msimu huu, mechi kati ya timu hizi mbili ilikamilika sare ya 2-2.

Thika  wanafunga tano bora kwenye jedwali na alama tisa. Tangia kujiuzulu kwa kocha Joseph Oyoo ambaye alijiunga na Mombasa Olympics, timu hiyo imekuwa ikisuasua ligini. Ikiwa timu hiyo haitaweza kushinda mechi zilizosalia za ligi, huenda wakashindwa kutetea taji lao msimu huu.

  • Tags

You can share this post!

Tottenham wasuka upya safu yao ya mbele kwa kusajili fowadi...

Uhispania wapewa Italia huku Uholanzi wakionana na Croatia...

T L