• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 2:08 PM
FAINALI YA FA: Ni Manchester United au Manchester City?

FAINALI YA FA: Ni Manchester United au Manchester City?

NA MASHIRIKA

MBIVU na mbichi kuhusu nani mkali kati ya Manchester City na Manchester United itajulikana watakapokabana koo katika fainali ya Kombe la FA ugani Wembley hivi leo Jumamosi.

Miamba hao wanakutana katika fainali kubwa kwa mara ya kwanza kabisa.

Takwimu za ana kwa ana kati ya majirani hao kwenye dimba hili zinaweka mashetani wekundu wa United juu kwani wamepata ushindi mara tano kati ya sita ambapo wamekutana ikiwemo 3-2 katika raundi ya 16-bora Januari 2012.

Mara moja ambayo City wamepiga United kwenye gozi hili ni 1-0 katika nusu-fainali mwaka 2011. Fainali hii itakuwa ya United ya 21 kwenye kipute hiki nao City wanashiriki fainali kwa mara yao ya 12.

Citizens wametwaa mataji sita ya Kombe la FA na kupoteza mara tano katika fainali katika makala 11 yaliyopita.

Mara ya mwisho walipofika fainali walibeba taji kwa kulipua Watford 6-0 mwaka 2019.

United wanaoshikilia rekodi ya kushiriki fainali mara nyingi kwa pamoja na Arsenal, wanawinda taji lao la 13. Pia, walibomoa City 2-1 mara ya mwisho walipoonana katika mashindano yoyote hapo Januari 14, 2023 ligini. Siku hiyo, Jack Grealish aliweka City kifua mbele dakika ya 60 kabla ya United kujibu kwa mabao kutoka kwa Bruno Fernandes na Marcus Rashford katika dakika 12 za mwisho.

Licha ya takwimu za ana kwa ana na pia ushindi wa United mara ya mwisho pande hizo zilikutana, City wanajivunia rekodi nzuri katika makombe ya nyumbani chini ya kocha Pep Guardiola. Mabingwa hao wa Ligi Kuu wanapigiwa upatu asilimia 100 ya kushinda makombe hayo tangu Mhispania Guardiola awasili msimu 2016-2017.

Msukumo

Wanatarajiwa kupata msukumo pia wa kupiga washindi wa Kombe la Carabao, United kutokana na kuwa wataweka hai matumaini ya kuwa timu ya pili kufagia mataji matatu katika msimu mmoja baada ya United kutawala Ligi Kuu, Kombe la FA na Klabu Bingwa Ulaya mwaka 1998-1999.

Hata hivyo, ni roho mkononi kwa City kwani karibu wachezaji watano wanauguza majeraha wakiwemo Grealish, Kevin De Bruyne na Ruben Dias.

Hata hivyo, kuna habari njema kwa mashabiki wa City. Nathan Ake na Aymeric Laporte wamepona majeraha.

Naye, Anthony Martial yuko nje ya kikosi cha kocha Erik Ten Hag baada ya kujeruhiwa. Macho yatakuwa kwa washambulizi Erling Haaland na Rashford kuongoza shughuli nzito ya kutafutia klabu zao za City na United ushindi, mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Kampeni ya FIFA ya kukuza soka ya wanawake nchini...

Pigo kwa Uhuru na Kioni, msajili wa vyama vya kisiasa...

T L