• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Kampeni ya FIFA ya kukuza soka ya wanawake nchini yakamilika washiriki wakituzwa

Kampeni ya FIFA ya kukuza soka ya wanawake nchini yakamilika washiriki wakituzwa

NA TOTO AREGE

KAMPENI ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kuimarisha kandanda ya wanawake imefika tamati Ijumaa katika uwanja wa Kasarani Annex jijini Nairobi.

Hafla hiyo ya siku mbili, imefika tamati kwa kishindo ikiongozwa na mwakilishi wa FIFA Sue Martin na Rais wa FKF Nick Mwendwa.

Bi Martin ni mtaalam wa programu ya maendeleo ya wanawake katika FIFA. Alipewa mgao wa kuja Kenya kusimamia na kusaidia kufanikisha mipango ya maendeleo ya FIFA katika FKF.

“Hongera sana FKF kwa kazi nzuri mnayofanya katika kukuza soka ya wanawake nchini Kenya na ambao wengi hufikia viwango vya kucheza nje ya nchi. Kwa miaka niliyokaa kwenye mchezo huo, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika soka ya wanawake,” akasema Bi Martin.

“FIFA ina msemo, ‘mpe kila mtu nafasi ya kucheza’. Haijalishi wewe ni mvulana au msichana, kila mtu anapaswa kupata fursa ya kucheza,” akaongeza.

Bw Mwendwa kwa upande wake amesisitiza sio tu kukuza soka ya wanawake uwanjani, bali pia kuandaa programu zaidi za ukocha na maendeleo ya waamuzi iliyoundwa mahususi kusaidia ushiriki wa wanawake nchini.

“Ningependa kushukuru FIFA kwa usaidizi wao katika kampeni hii. Nawaomba wadau wote wakiwemo wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuunga mkono juhudi zetu za kukuza soka ya wanawake nchini Kenya. Tunaamini kuwa kampeni hii itatusaidia kufikia lengo letu la kufuzu kwa Kombe la Dunia la wanawake mwaka wa 2027,” amesema Mwendwa.

Kampeni hiyo ni programu ya kimataifa inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika soka na kukuza maendeleo ya wanawake katika mchezo huo.

Hafla hiyo ilianza Alhamisi wiki hii na ilileta pamoja timu 30 na timu 32 kutoka shule za msingi kutoka matawi ya FKF ya Nairobi Magharibi na Nairobi Mashariki mtawalia.

Baada ya uzinduzi rasmi, timu hizo pia zilihusishwa katika kucheza soka ya wachezaji sita kila upande.

Mechi hizo zilikusudiwa kuunda mazingira ya kufurahisha na ya kuvutia kwa watoto.

Zaelyn Academy kutoka Nairobi Magharibi na Shule ya Msingi ya St Martins kutoka Nairobi Mashariki ndio mabingwa wa jumla wa mashindano hayo. Timu zote 62 zilipokea mipira minne minne kwa kila moja.

  • Tags

You can share this post!

Riadha za Dunia Budapest: Kiptum na Kosgei kuongoza timu ya...

FAINALI YA FA: Ni Manchester United au Manchester City?

T L