• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Pigo kwa Uhuru na Kioni, msajili wa vyama vya kisiasa akidinda kuidhinisha maamuzi ya NDC

Pigo kwa Uhuru na Kioni, msajili wa vyama vya kisiasa akidinda kuidhinisha maamuzi ya NDC

NA CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine juhudi za Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kurejesha udhibiti wake wa chama cha Jubilee zimepata pigo baada ya msajili wa Vyama Vya Kisiasa Anne Nderitu kudinda kuidhinisha maafisa wapya walioteuliwa Mei.

Maafisa hao wapya waliteuliwa katika kongamano maalum la wajumbe wa Jubilee (NDC) lililofanyika Mei 22, 2023 katika uwanja wa Ngong’ Racecourse.

Hii ni baada ya mkutano huo kuwafurusha maafisa waasi wakiongozwa na mkurugenzi wa uchaguzi Kanini Kega, mwenyekiti wa kitaifa Nelson Dzuya, naibu katibu mkuu Joshua Kuttuny na wabunge Sabina Chege na Rachel Nyamai (Kitui Kusini) na wabunge wa zamani Dkt Naomi Shabaan na Jimmy Angwenyi.

Bi Nderitu pia alidinda kuwaidhinisha maafisa wapya walioteuliwa katika NDC hiyo kuchukua nafasi za maafisa waliofurushwa.

Miongoni mwao ni aliyekuwa Katibu wa Wizara katika Idara ya Mipango Saitoti Torome aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa kitaifa kuchukua nafasi ya Bw Dzuya, Bw Yasin Noor aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu kuchukua nafasi ya Bw Kuttuny na aliyekuwa Mbunge wa Kigumo Jamleck Kamau aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uchuguzi kuchukua nafasi ya Bw Kega ambaye pia ni mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).

Chama cha Jubilee pia kilimteua mwanablogu Bi Pauline Njoroge kuwa naibu katibu mpanga ratiba.

Kongamano hilo ambalo liliongozwa na Bw Kenyatta mwenyewe na kuhudhuriwa na vinara wengine wa Azimio kama vile Raila Odinga, Martha Karua na Kalonzo Musyoka, pia liliamua kwamba wabunge wa Jubilee ambao wameamua kushirikiana na mrengo wa Kenya Kwanza wafurushwe chamani.

Maamuzi hayo yaliwasilishwa kwa afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni mnamo Mei 23, 2023.

Lakini kwenye barua yake aliyoandikia chama hicho Mei 29, 2023, Bi Nderitu ameitisha orodha ya wajumbe waliohudhuria NDC kabla ya afisi yake kuidhinisha maamuzi ya kongamano hilo.

“Baada ya kukagua stakabadhi zilizowasilishwa, afisi hii haiwezi kushughulikia maamuzi kutokana na ukosefu wa stakabadhi nyingine hitajika,” akasema Bi Nderitu katika barua yake kwa Bw Kioni.

Miongoni mwa stakabadhi ambazo Bi Nderitu anahitaji ni orodha ya wajumbe waliohudhuria NDC ikiandamanishwa na nambari zao za vitambulisho.

“Hii itaisaidia afisi hii kuthibitisha wale waliohudhuria mkutano huo na ikiwa NDC hiyo ilitimiza hitaji la kipengele cha 8.1 (1) na 23 cha Katiba ya Jubilee,” Bi Nderitu akasema.

Afisi ya Bi Nderitu pia inataka kumbukumbu za mkutano huo wa NDC ili ibaini uhalali wa mbinu za uchaguzi zilizotumiwa kuwachagua maafisa hao wapya wa kitaifa wa Jubilee.

Stakabadhi hizo zinahitajika ili kubaini ikiwa kongamano hilo lililofanyika Mei 22 liliandaliwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Aidha, afisi hiyo inataka kubaini ikiwa kubadilishwa kwa mahala pa mkutano kutoka Bomas of Kenya hadi Ngong’ Racecourse kulifanywa kwa kuzingatia kanuni iliyowekwa.

Hatua ya Bi Nderitu kumpiga breki maamuzi hayo inaashiria kuwa kufurushwa kwa akina Kega, Chege, Dzuya na wengine hakuwezi kutekelezwa.

  • Tags

You can share this post!

FAINALI YA FA: Ni Manchester United au Manchester City?

Kocha Sam Allardyce abanduka kambini mwa Leeds United

T L