• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Familia ya Alvaro Morata yatishiwa maisha baada ya kupoteza nafasi nyingi za kufungia Uhispania mabao kwenye Euro

Familia ya Alvaro Morata yatishiwa maisha baada ya kupoteza nafasi nyingi za kufungia Uhispania mabao kwenye Euro

Na MASHIRIKA

FOWADI Alvaro Morata wa Juventus ameshikilia kwamba familia yake ilitishiwa maisha na watu wasiojulikana jijini Seville kwa sababu ya kushindwa kufungia Uhispania mabao muhimu kwenye mechi zinazoendelea za Euro.

“Watu wamekuwa wakitaka watoto wangu wafe. Ningependa nao wajiweke katika hali yangu na kuhisi uchungu ninaopitia hasa familia yako inapotishiwa maisha kwa sababu ya mpira,” akasema Morata kwenye mahojiano na kituo cha Cadena Cope nchini Uhispania.

“Mke wangu na watoto wamekuwa wakija uwanjani kushabikia Uhispania wakiwa wamevalia jezi zenye jina ‘Morata’ mgongoni,” akaendelea.

“Inatia hofu kwamba wao huzomewa na kutishiwa maisha kwa namna mbalimbali mwishoni mwa mechi. Najua wachezaji huzomewa na mashabiki kila wanapopoteza nafasi za wazi uwanjani, lakini kuna mipaka pia,” akaelezea.

Morata ambaye anachezea Juventus kwa mkopo kutoka Atletico Madrid, alipoteza nafasi nyingi za wazi kwenye mechi tatu zilizopigwa na Uhispania katika Kundi E, ikiwemo penalti aliyopoteza katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Slovakia mnamo Juni 23, 2021.

Alizomewa na kurushiwa cheche za maneno katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha Uhispania na Ureno mnamo Mei 2021. Alijipata katika presha zaidi katika sare tasa iliyosajiliwa na Uhispania dhidi ya Uswidi katika mechi ya kwanza ya Kundi E kwenye Euro kabla ya mabingwa hao wa 2008 na 2012 kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Poland.

Ingawa alifunga bao dhidi ya Poland, Morata alipoteza nafasi kadhaa za wazi, ikiwemo ile iliyotokana na penalti ya Gerard Moreno kugonga mhimili wa goli na mpira kurejea uwanjani.

Ushindi wa 5-0 dhidi ya Slovakia uliwakatia Uhispania tiketi ya hatua ya 16-bora ambapo sasa watamenyana na Croatia mnamo Juni 28, 2021.

Uhispania waliokamata nafasi ya pili kwenye Kundi E, watapimana ubabe na Croatia ambao pia walikamilisha kampeni za Kundi D katika nafasi ya pili.

Croatia waliozidiwa maarifa na Ufaransa kwenye fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018, walibanduliwa kwenye hatua ya 16-bora ya Euro mnamo 2016. Walifungua kampeni za Kundi D kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Uingereza kabla ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech na kulaza Scotland 3-1 hatimaye.

Uhispania walitawazwa mabingwa wa Euro mnamo 1964, 2008 na 2012; na wakaibuka wafalme wa Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jamhuri ya Czech yaduwaza Uholanzi na kujikatia tiketi ya...

Ecuador wapiga breki rekodi ya Brazil kwa kuwalazimishia...