• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 3:09 PM
Fati arejea kikosini na kuwabeba Barcelona dhidi ya Levante ligini

Fati arejea kikosini na kuwabeba Barcelona dhidi ya Levante ligini

Na MASHIRIKA

BARCELONA walimpunguzia kocha Ronald Koeman presha ya kutimuliwa baada ya kupokeza Levante kichapo cha 3-0 katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) uwanjani Camp Nou.

Penalti ya dakika ya sita kutoka kwa Memphis Depay iliwaweka Barcelona kifua mbele baada ya fowadi huyo raia wa Uholanzi kuchezewa visivyo na Nemanja Radoja.

Mholanzi Luuk de Jong alifungia Barcelona goli la pili baada ya kushirikiana vilivyo na Sergino Dest. Bao la De Jong lilikuwa lake la kwanza ndani ya jezi za Barcelona tangu asajiliwe na miamba hao kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Sevilla.

Ansu Fati aliyekuwa akirejea kuchezea Barcelona baada ya kuwa nje kwa kipindi kirefu kuuguza jeraha alipachika wavuni bao la tatu.Ushindi huo uliwapaisha Barcelona hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la La Liga huku pengo la pointi tano likitamalaki kati yao na viongozi Real Madrid.

Presha ya kufutwa kazi kwa Koeman iliongezeka wiki jana baada ya Barcelona kushinda mechi mbili pekee kati ya tano za ufunguzi wa kampeni za La Liga muhula huu.

Masogora wa Barcelona walijituma ipasavyo dhidi ya Levante licha ya kukosa Koeman aliyekuwa akitumikia marufuku baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu katika mechi ya awali iliyomalizikia kwa sare tasa dhidi ya Cadiz.

Levante hawakuelekeza kombora lolote langoni mwa Barcelona hadi dakika ya 81. Naye Depay alipoteza nafasi nyingi za wazi za kumzidi maarifa kipa Aitor Fernandez.

Fati, 18, alikuwa akirejea katika kikosi cha Barcelona akivalia jezi nambari 10 mgongoni iliyokuwa ya Lionel Messi ambaye sasa anachezea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

Mechi dhidi ya Levante ilikuwa ya kwanza kwa chipukizi huyo aliye na usuli nchini Guinea-Bissau kuchezea Barcelona tangu Novemba 2020 alipofanyiwa upasuaji wa goti.

  • Tags

You can share this post!

Juventus waingia ndani ya 10-bora jedwalini baada ya...

Morogo akana kituo cha polisi cha Syokimau kilikuwa na seli