• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:44 PM
FENCING: Alexandra Ndolo ajizolea sifa kwa kupigana kwa upanga

FENCING: Alexandra Ndolo ajizolea sifa kwa kupigana kwa upanga

NA AREGE RUTH

MCHEZO wa kupigana kwa upanga, maarufu kwa Kimombo kama fencing, bado haujashika mizizi nchini Kenya lakini ni miongoni mwa michezo mikongwe zaidi duniani.

Huu ni mchezo wa kivita ambao unatumia upanga mwembamba wa kupinda, na unahusisha wachezaji wawili pekee. Kuna vitengo vitatu: Foil, Épée na Sabre, huku kila kimoja kikitumia aina tofauti ya upanga na sheria zake.

Alexandra Ndolo ni mchezaji bora nambari 10 duniani katika fencing, na wa kwanza barani Afrika.

Ndolo, 36, ni mzaliwa wa Ujerumani katika eneo la Bayreuth kaskazini mwa mji wa Bavaria, ambako alilelewa na pia kujifahamisha kuhusu mchezo huo.

Shughuli za kazi zilifanya babake – raia wa Kenya (sasa marehemu) – na mamake wa kutoka Poland kuhamia huko Ujerumani ambako Ndolo alizaliwa. Kwa asili ya kuzaliwa huko alipata fursa ya kuwakilisha Ujerumani katika mashindano mbalimbali.

Mkenya ALexandra Ndolo ambaye ni gwiji wa mchezo wa kutumia upanga ‘Fencing’ akiwa kwenye ziara nchini Italy mnano Septemba 27, 2022.
PICHA /HISANI/

Hata hivyo, baada ya miaka 15 sasa amebadilisha uraia wake hadi Kenya; hatua iliyofanywa rasmi mnamo Septemba iliyopita.

Moja ya sababu za kubadili uraia ni kupata nafasi ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa, mwaka 2024; kule Ujerumani ushindani ni mkali na kupata fursa timuni ni nadra.

Pia, lengo lake ni kuanzisha na kukuza fencing hapa nchini Kenya. Kando na Olimpiki, Ndolo pia atawakilisha Kenya katika mashindano yoyote ya kimataifa ya fencing. Mkenya huyo ni hodari mno kutumia mkono wa kushoto katika kitengo cha Épée – hapa mchezaji hutumia silaha kubwa na nzito zaidi ya vitengo vingine. “Nimerejea nyumbani alikotoka babangu na ilipo nusu ya familia yangu.

Hapa ni nyumbani,” alisema kwenye mahojiano na Dimba majuzi. “Pia, ninahisi nafasi yangu ya kufuzu kwa michezo ya Paris mwakani ni kubwa sana nikiwa Kenya,” aliongeza mshindi huyo wa medali ya fedha (2017) na shaba (2019) mashindano ya bara Ulaya. Aidha, mwaka jana alizoa fedha kitengo cha Epée wakati wa mashindano ya dunia jijini Cairo, Misri. Kwa jumla ameshiriki makombe sita ya dunia ambayo anaamini yamempa tajriba tosha.

“Nina imani na Kenya na pia najiamini. Nina hamu ya kushinda na ninataka kudhihirisha kwamba inawezekana Kenya kuwa bingwa wa fencing,” alihoji.

Wakati hayuko vitani kispoti Ndolo alikuwa akihusika na vita vingine kama afisa katika jeshi la Ujerumani ili kupata ujira wa kukidhi mahitaji yake. Anaomba wafadhili kujitokeza kumpa sapoti Kenya.

“Mchezo huu ni ghali mno na changamoto kuu ni ufadhili. Naomba wafadhili wajitokeze,” alirai.

Kwa sasa anazidi kueneza injili ya fencing mashinani kupitia mafunzo kwa chipukizi na klabu ya gofu ya Karen Golf Club. Ndolo pia ndiye mwanzilishi wa Shirikisho la Fencing Kenya.

Zaidi, anatumai fencing itaorodheshwa kuwa mojawapo ya michezo mengine na Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki-Kenya (NOC-K), ili Kenya iwe na uwakilishwa wake Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa.

  • Tags

You can share this post!

NYOTA WA WIKI: Kevin de Bruyne

Chepng’etich kivutio Istanbul Half Marathon nchini...

T L