• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:50 AM
NYOTA WA WIKI: Kevin de Bruyne

NYOTA WA WIKI: Kevin de Bruyne

NA GEOFFREY ANENE

HAKUNA mjadala kuhusu weledi wa Kevin De Bruyne kama mmoja wa viungo stadi katika ulimwengu wa soka.

Kazi yake safi safu ya kati na mbele imefanya apate umaarufu mkubwa kiasi cha kutajwa na wadau wa soka kuwa kiungo namba wani duniani.

Amejizolea mataji mengi ya kibinafsi ikiwemo kuibuka Mchezaji Bora wa Mwaka kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na pia Mchezaji Mbunifu Bora wa msimu mara mbili.

De Bruyne, aliyekamata nafasi ya tatu kwenye tuzo ya kifahari ya Mwanasoka Bora Duniani (Ballon d’Or) mwaka 2022, amejinadi kwa wapenzi wa soka kwa kusuka pasi za uhakika, kuchanja krosi hatari na pia katika kusukumia makipa makombora motomoto.

Timu ya hivi punde kuonja makali yake ni wanabunduki wa Arsenal wiki hii. De Bruyne alimwaga kipa wa Arsenal, Aaron Ramsdale, mara mbili Cityzens wakiwika 4-1 ugani Etihad mnamo Jumatano, katika mechi itakayochangia pakubwa kuamua nani atabeba taji la EPL msimu huu. Mwanasoka huyo, ambaye ni mzuri kwa kutumia miguu yote, alilelewa mjini Ghent, Ubelgiji. Alianza kucheza soka akiwa na umri wa miaka minne pekee.

Alikuzwa katika klabu za KVV Drongen na Gent kabla kujiunga na Genk mwaka 2005. Alianzia soka yake ya watu wazima kambini mwa Genk waliompa kandarasi ya kwanza ya kulipwa mnamo 2008.

Kutoka hapo, De Bruyne alichezea Chelsea iliyompeleka Werder Bremen katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mkopo. Kisha wakamuuza kabisa kwa Wajerumani wengine Wolfsburg kwa kima cha Sh3.2 bilioni.

Manchester City ilimsaini kwa ada ya Sh11.3 bilioni mwaka 2015. Sifa nyingine zinazofanya De Bruyne kuvuma ni uwezo wa kuona wachezaji wenza walivyojipanga uwanjani. Pia uwezo wa kutumiwa kama winga ama mshambulizi wa pili. De Bruyne pia ni mkali katika kupiga chenga. Kimataifa, De Bruyne alichagua kuwakilisha Ubelgiji, ingawa alikuwa pia na fursa ya kuvalia jezi ya Burundi ambako mamake Anna alizaliwa.

De Bruyne amechezea Ubelgiji kutoka timu ya taifa ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 hadi sasa. Mechi yake ya kwanza katika timu ya watu wazima ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Finland mnamo 2010. Anachokosa tu na timu ya taifa ni mataji.

Amechezea timu ya watu wazima jumla ya mechi 99 akifunga mabao 26 na kuchangia pasi 48 zilizojazwa kimiani. De Bruyne, ambaye alifanywa nahodha wa Ubelgiji mwezi Machi, ameoa Michele Lacroix na wamebarikiwa na watoto watatu. Rekodi Yake DE Bruyne anashikilia rekodi ya mchezaji aliyefikisha pasi zilizozalisha magoli 100 kwa haraka.

Alipata rekodi hiyo katika mechi yake ya 237 alipomegea Erling Haaland pasi wakati Manchester City ililima Southampton 4-1 mapema mwezi huu. Kiungo huyo mpakuaji wa Ubelgiji alimpiku Mhispania Cesc Fabregas aliyepata idadi hiyo ya pasi katika mechi 293.

De Bruyne pia yuko saka kwa bako na jagina wa Arsenal, Thierry Henry, katika uchangiaji wa pasi nyingi zilizozaa magoli katika msimu mmoja wa EPL (20). Alipata rekodi hiyo msimu 2019-2020.

Isitoshe, De Bruyne analipwa mshahara wa juu kabisa kwenye EPL, ingawa inaaminika kuwa Haaland anampiku kwa mapato marupurupu yanapoongezwa.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Suluhu ya kudumu Sudan itatoka Afrika si...

FENCING: Alexandra Ndolo ajizolea sifa kwa kupigana kwa...

T L