• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
FKF yampa kocha mpya miezi 2 tu

FKF yampa kocha mpya miezi 2 tu

Na CECIL ODONGO

MASHABIKI wa soka nchini Jumapili walishangazwa na hatua ya Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa kumpa kocha mpya wa Harambee Stars Engin Firat mkataba wa miezi miwili pekee.

Wakati wa kikao cha kumtambulisha rasmi kocha huyo katika hoteli ya Safari Park, Mwendwa alisema Firat mwenye umri wa miaka 51, ana kibarua kigumu cha kuhakikisha Kenya inashinda mechi zake nne za kufuzu Kombe la Dunia.

Firat alikuwa na rekodi duni katika timu ya taifa ya Moldovia ambako alihudumu kwa miaka miwili kabla ya kujiuzulu mapema mwaka 2021.

Alisimamia mechi 11 ila hakushinda yoyote, akapata sare mbili na kushindwa mara tisa.

Mwendwa alisema FKF itaaamua kuagana na kocha huyo au kumpa mkataba mrefu kutokana na matokeo ya mechi hizo za kufuzu Kombe la Dunia.

“Nawatambulisheni Firat, kocha mwenye uzoefu mkubwa wakati ambapo Kenya inalenga kumaliza kileleni mwa kundi lao. Ana tajriba pana na alisimamia Moldova ikicheza dhidi ya timu zilizoshamiri kwenye soka kama Ufaransa na Italia,” akasema Mwendwa.

“Tumeamua kumpa mkataba wa miezi miwili ili asimamie mechi zetu nne za kufuzu Kombe la Dunia kisha kutegemea na matokeo atakayoyapata ndipo tutaamua kuendelea naye au kuagana naye baada ya muda huo kukamilika,” akaongeza Mwendwa.

Kenya inatarajiwa kuchuana na Mali mnamo Oktoba 6 nyumbani kisha Oktoba 12 ugenini kabla ya kuvaana na Uganda mnamo Novemba 11 kisha itamatishe mechi za makundi dhidi ya Rwanda Novemba 14.

Kwa upande wake, Firat alitetea rekodi yake mbovu akisimamia Moldova, na kusema kuwa mechi alizokuwa akishiriki na timu ya taifa hilo zilikuwa dhidi ya timu ngumu ambazo zimetawala soka ya Uropa kwa miaka mingi.

Kulingana na orodha inayotolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Moldova inashikilia nambari 175 huku Kenya ikiwa nafasi ya 104.

“Nafurahia kuwa Kenya na nafahamu malengo mazito ambayo yako mbele yangu. Kenya ni taifa ambalo linapenda soka ikilinganishwa na Moldova na nina wingu la matumaini nitatimizi malengo haya,” akasema.

Kando na Moldova, timu nyingine ambazo Firat amesimamia ni Eintracht Frankfurt ya Ujerumani na Fenerbahce ya Uturuki.

You can share this post!

Pendekezo barabara ya jiji la Nairobi ipewe jina la Raila

STEPHEN JACKSON: Mifumo thabiti ya lishe kufaa uchumi na...