• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
Florence Diamond League: Chepng’etich afuta rekodi ya dunia ya Dibaba

Florence Diamond League: Chepng’etich afuta rekodi ya dunia ya Dibaba

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Faith Chepng’etich Kipyegon ametimiza ndoto yake ya kumiliki rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500, huku Ferdinand Omanyala akimaliza katika nafasi ya pili kwenye mbio za umbali wa mita 100 wakati wa mashindano ya riadha za Florence Diamond League mnamo Juni 2 usiku.

Chepng’etich, ambaye kwa karibu miaka miwili hajakuwa na kifani katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara nne, alitwaa taji kwa dakika 3:49.11. Alifuta rekodi ya 3:50:07 iliyowekwa na Muethiopia Genzebe Dibaba mwaka 2015.

Bingwa huyo mara mbili wa dunia na Olimpiki, ambaye hufanya mazoezi na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon Eliud Kipchoge, amekuwa na lengo la kuweka rekodi ya dunia ya 1,500m kwa muda sasa.

“Rekodi ya dunia ya 1,500m inawezekana,” alisema baada ya kukosa rekodi ya Dibaba pembemba akishinda Monaco Diamond League kwa 3:50.37 mwezi Agosti 2022.

Alianza msimu huu wa Diamond League kwa kutawala duru ya Doha, Qatar kwa dakika 3:58.57 mnamo Mei 5 na kuahidi kabla ya ziara ya Florence kuwa huenda 2023 ndio mwaka wa kuandikisha matokeo yake bora zaidi katika 1,500m.

Hapo Ijumaa, Chepng’etich aliwekewa kasi na Waamerika Brooke Feldmeier na Sage Hurta-Klecker wanaoshiriki mbio za mita 800.

Feldmeier alimwongoza kukamilisha mita 400 za kwanza kwa sekunde 62.37 kabla ya Hurta-Klecker kuchukua usukani katika mzunguko wa pili na kumsaidia kuukamilisha kwa sekunde 61.63. Waamerika wote wawili walibanduka na kusalia kutazama mizunguko miwili ya mwisho Chepng’etich akikamilisha 1,200 kwa 3:05.20 kabla ya kukamilisha mita 400 za mwisho kwa 58.81.

Mwingereza Laura Muir aliridhika na nafasi ya pili kwa 3:57.09 naye Jessica Hull akaweka rekodi mpya ya Australia akifunga nafasi tatu za kwanza kwa 3:57.29.

Bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola mbio za mita 100 Omanyala alimaliza katikati ya Waamerika Fred Kerley na Trayvon Bromell. Mshindi wa dunia Kerley alikata utepe kwa sekunde 9.94 akifuatiwa na Omanyala (10.05), Bromell (10.09), raia wa Afrika Kusini Akani Simbine (10.09) na Mwitaliano Samuele Ceccarelli (10.13).

  • Tags

You can share this post!

Kocha Sam Allardyce abanduka kambini mwa Leeds United

Serikali yatenga Sh130 milioni kupiga jeki kilimo cha miraa

T L