• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Francois Msafiri atimka saa 26 kutoka Eldoret hadi Nairobi kuhubiri amani

Francois Msafiri atimka saa 26 kutoka Eldoret hadi Nairobi kuhubiri amani

NA GEOFFREY ANENE

MKIMBIAJI wa mbio ndefu za zaidi ya kilomita 42, Francois Msafiri alikamilisha mbio za kilomita 320 kutoka Eldoret hadi Nairobi jana Jumapili.

Mkimbizi huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alitoka stani ya magari ya North Rift saa kumi na mbili na dakika 31 Jumamosi asubuhi akipitia njia ya Kaptagat na kufika Nairobi nje ya uwanja wa kitaifa wa Nyayo saa tatu kasoro dakika 12 asubuhi jana.

Msafiri alitumia saa 26 na dakika saba kukamilisha umbali huo, lengo lake likiwa ni kuhamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa kudumisha amani.

“Ninajivunia kuwa misheni yangu ya kuhamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa amani imekamilika,” alisema Msafiri aliyetimka kilomita 512 kutoka Nairobi hadi Mombasa mwaka 2021 na pia kilomita 155 kutoka Eldoret hadi Nakuru mwezi Februari 2022.

Msafiri anasema alichagua kuanzia mbio hizo Eldoret kwa sababu mji huo unafahamika kama ‘nyumbani’ kwa mabingwa.

“Pia jamii ya Eldoret inathamini sana riadha. Isitoshe, Eldoret inapatikana katika eneo la miinuko ambalo lina hali nzuri ya anga ya kukimbia,” alieleza Msafiri aliyejikakamua kukamilisha mbio hizo licha ya kupata kidonda katika mguu wake wa kushoto alipofika eneo la Gilgil.

Aliombewa baada ya kufika mtaani Syokimau anakoishi.

  • Tags

You can share this post!

Uingereza yazama, Ujerumani ikila sare

PAUKWA: ‘Mshahara’ wa funguo wamkera sana Madhila

T L