• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
PAUKWA: ‘Mshahara’ wa funguo wamkera sana Madhila

PAUKWA: ‘Mshahara’ wa funguo wamkera sana Madhila

NA ENOCK NYARIKI

SIKU iliyofuata, asubuhi mbichi, Madhila aliubisha mlango wa mwajiri wake. Hakuwa na shaka kuhusu suala la kuonana naye.

Bwana Kizito alikuwa na mazoea ya kurauka asubuhi na mapema kuliko mtu mwingine katika kiambo kile. Alipoufungua mlango, alikabiliana uso kwa macho na mfanyakazi wake ambaye alikuwa amebeba kifurushi tayari kuondoka.

“Kijana, wakati wote umeishi nyumbani kwangu, haikuwahi kutokea siku moja nikakufukuza kazini. Mbona basi leo umenijia asubuhi na mapema kana kwamba nimekufukuza?’’ Bwana Kizito aliuliza.

“Samahani bosi, unajua kwamba kwetu ni maporini tena usafiri ni tabu,’’ Madhila alisema kwa unyenyekevu.

Tabasamu lilichanua kwenye kipaji cha Bwana Kizito. Alirudi ndani ya nyumba na kurejea na kicha cha funguo akamkabidhi Madhila. Madhila alipothibitisha kuwa mwajiri wake hakuwa na kitu kingine zaidi ya zile funguo, alipigwa na butwaa. Midomo ikimchezacheza kama aliyetaka kusema jambo. Kama aliyeyasoma mawazo ya Madhila, Kizito alisema:

“Funguo hizo zitakufaa. Kumbuka kwamba subira ni ufunguo wa milango ya heri.”

Maneno yale yalimchoma Madhila moyoni kama usena wa nyuki. Alitarajia kupewa pesa ambazo bwana wake alimwia baada ya miaka kadhaa ya kumlipa mshahara nusu nusu kama nyama ya mbuzi.

Sasa tazama alichomkabidhi badala yake: kicha cha funguo! Je, atakitumia kicha cha funguo kama nauli? Akifika nyumbani, watoto wake watakula kicha cha funguo? Maswali chungu mbovu yalimtambaa mawazoni.

HADITHI ITAENDELEA

  • Tags

You can share this post!

Francois Msafiri atimka saa 26 kutoka Eldoret hadi Nairobi...

MWALIMU WA WIKI: Theuri ni mwalimu mfano wa jungu kuu

T L