• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 9:50 AM
Uingereza yazama, Ujerumani ikila sare

Uingereza yazama, Ujerumani ikila sare

Na MASHIRIKA

UINGEREZA walianza kampeni zao za Uefa Nations League kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Hungary jijini Budapest mnamo Jumamosi huku Ujerumani ambao ni mabingwa mara nne wa dunia wakilazimishia chipukizi wa Italia sare ya 1-1 katika uwanja wa Renato Dall’Ara mjini Bologna.

Nyota wa RB Leipzig, Dominik Szoboszlai, alifungia Hungary penalti ya kipindi cha pili baada ya Reece James kumchezea Zsolt Nagy visivyo. Ilikuwa mara ya kwanza tangu 1962 kwa Hungary kuangusha Uingereza.

Hadi waliposhuka dimbani, Uingereza hawakuwa wamepoteza mechi yoyote kati ya 22 za awali isipokuwa kichapo cha penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1 katika fainali ya Euro mnamo Julai 2021 ugani Wembley.

Mara ya mwisho kwa Uingereza kupigwa chini ya dakika 90 za mchezo ni Novemba 2020 walipotandikwa na Ubelgiji 2-0 katika gozi la Nations League.

“Fainali zilizopita za Euro zilitupa jukwaa la kudhihirisha ukubwa wa uwezo wetu dhidi ya miamba. Ushindi huu unatosha kusadikisha mashabiki wetu. Kibarua kizito kikubwa kilichoko mbele ni kuendeleza ubabe huo,” akasema nahodha wa Hungary, Adam Szalai.

Uingereza waliowajibisha beki James Jutsin (Leicester City) na fowadi Jarrod Bowen (West Ham United) kwa mara ya kwanza, walikosa kutamba huku Bukaya Saka (Arsenal) na Harry Kane (Tottenham Hotspur) wakipoteza nafasi nyingi za wazi. Pambano hilo lilihudhuriwa na mashabiki 30,000, asilimia kubwa ikiwa wanafunzi.

“Yasikitisha kwamba tulipoteza licha ya kutamalaki mechi na kumiliki asilimia kubwa ya mpira. Zaidi ya joto jingi, uchovu pia ulichangia kushindwa kwetu. Msimu ulikuwa mrefu na baadhi ya masogora wetu waliwajibishwa na klabu zao katika takriban mechi zote za muhula huu,” akasema kocha Gareth Southgate.

Mechi hiyo ilitarajiwa kusakatwa bila mashabiki baada ya mashabiki wa Hungary kuzua fujo wakati wa michuano yao kwenye fainali za Euro 2020. Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Hungary lilichuma nafuu kutokana na kanuni za UEFA zilizokubalia watoto wasiozidi umri wa miaka 14 kuhudhuria kipute hicho bila ada.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ruto, Raila wapatana kuhusu masuala IEBC

Francois Msafiri atimka saa 26 kutoka Eldoret hadi Nairobi...

T L