• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Ghana yabandua Nigeria na kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022

Ghana yabandua Nigeria na kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

GHANA ilikuwa timu ya kwanza ya Afrika kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar baada ya kulazimishia Nigeria sare ya 1-1 jijini Abuja na kusonga mbele kwa kanuni ya bao la ugenini.

Hata hivyo, mashabiki wa Nigeria walizua vurugu mwishoni mwa mechi hiyo kwa kurushia wachezaji na maafisa wa Ghana chupa za maji walipokuwa wakiondoka uwanjani. Kiungo mkabaji wa Arsenal, Thomas Partey aliwaweka Ghana kifua mbele katika dakika ya 10 kabla ya beki wa Watford, William Trost-Ekong kusawazisha mambo kupitia penalti baada ya Ademola Lookman kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku.

Ghana na Nigeria walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo ya marudiano baada ya kuambulia sare tasa katika mkondo wa kwanza jijini Kumasi mnamo Machi 25, 2022. Black Stars ya Ghana haikufuzu kwa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi. Kwa kudengua Nigeria, Super Eagles walinyimwa nafasi ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya nne mfululizo.

Nigeria sasa hawajawahi kushinda Ghana katika mechi yoyote kati ya tano zilizopita tangu wawapepete 1-0 mnamo 2006. Ghana walishuka dimbani wakijivunia rekodi ya kushinda michuano 21, kusajili sare mara 19 na kupoteza mechi 10 kati ya 50 za awali dhidi ya Nigeria.

Kwa upande wao, Nigeria hawakuwa wameshindwa katika michuano sita mfululizo hadi Tunisia walipowadengua kwenye hatua ya 16-bora ya AFCON kwa kichapo cha 1-0 mnamo Januari 23 nchini Cameroon. Nigeria ambao ni mabingwa mara tatu wa Afrika walikuwa wakilenga kunogesha Kombe la Dunia mara sita huku Ghana wakifuzu sasa kuwakilisha Afrika duniani kwa mara ya nne baada ya kusakata fainali za 2006, 2010 na 2014.

You can share this post!

Bruno Fernandes abeba Ureno hadi fainali za Kombe la Dunia...

Ufaransa wakomoa Afrika Kusini huku Giroud akikaribia...

T L