• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Bruno Fernandes abeba Ureno hadi fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar

Bruno Fernandes abeba Ureno hadi fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar

Na MASHIRIKA

KIUNGO mvamizi wa Manchester United, Bruno Fernandes, alifunga mabao mawili na kusaidia timu ya taifa ya Ureno kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia baada ya kupepeta Macedonia Kaskazini 2-0 katika fainali ya mchujo mnamo Jumanne usiku.

Mabao hayo ya Fernandes yalichangiwa na Cristiano Ronaldo na Diogo Jota mtawalia katika mchuano huo uliosakatiwa jijini Porto. Hata hivyo, Macedonia Kaskazini walianza mechi kwa matao ya juu huku wakimwajibisha vilivyo kipa wa Ureno, Diogo Costa.

Huku Ureno wakifuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya sita mfululizo, nguli Cristiano Ronaldo atakuwa akinogesha kipute hicho cha haiba kubwa kwa mara ya tano ambayo huenda ndiyo ikawa yake ya mwisho kitaaluma sawa na hali ilivyo kwa Pepe, 39 na Joao Moutinho, 35.

Ureno wanaonolewa na kocha Fernando Santos walishuka ugani Do Dragao wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-1 kwenye nusu-fainali iliyowakutanisha na Uturuki mnamo Machi 24, 2022. Kwa upande wao, Macedonia Kaskazini walikuwa na kiu ya kuendeleza historia baada ya kuzamisha Italia 1-0 kwenye nusu-fainaili jijini Palermo na kunyima mabingwa hao wa bara Ulaya fursa ya kunogesha Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo.

Ureno hawajawahi kukosa kunogesha fainali za kipute chochote cha haiba kubwa tangu 1998 waliposhindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia baada ya kuambulia nafasi ya tatu kwenye kundi lililojumuisha Ujerumani, Ukraine na Armenia.

Mabingwa hao wa Euro 2016 wamefunga bao katika mechi zote 20 zilizopita za kufuzu kwa Kombe la Dunia tangu waambulie sare tasa dhidi ya Uswidi mnamo Machi 2009. Ureno na Macedonia Kaskazini waliwahi kukutana mara ya mwisho mnamo 2012 katika mchuano wa kupimana nguvu uliokamilika kwa sare tasa jijini Porto.

You can share this post!

Poland yapepeta Uswidi na kujikatia tiketi ya kuelekea...

Ghana yabandua Nigeria na kufuzu kwa fainali za Kombe la...

T L