• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Ismael Dunga ni mali ya Sagan Tosu kwenye Ligi Kuu ya Japan

Ismael Dunga ni mali ya Sagan Tosu kwenye Ligi Kuu ya Japan

Na GEOFFREY ANENE

JE, Ismael Salim Dunga ataweza kufuata nyayo za mshambuliaji mwenzake Michael “Engineer” Olunga?

Hilo ndilo swali kubwa ambalo mashabiki wa Ligi Kuu ya Japan watatumai Dunga atafaulu kujibu baada ya kujiunga na Sagan Tosu mnamo Januari 25, 2021, kwa kandarasi ya mwaka mmoja itakayokatika Januari 31, 2022.

Sagan Tosu imethibitisha kusaini Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 27 kutoka viongozi wa Ligi Kuu ya Albania, Vllaznia baada ya kuchapisha habari za uhamisho wake kwenye tovuti yake pamoja na mitandao yake ya kijamii.

Imesema kuwa “Ismael Dunga amejiunga nasi kikamilifu”, ingawa haijafichua urefu wa kandarasi yake, ada iliyolipwa ama mshahara wake.

Dunga, ambaye amekuwa Albania tangu mwaka 2018 akivalia jezi ya Luftetari (kutoka Agosti 2018), KF Tirana (2019) na Vllaznia, alithibitisha kununuliwa kwake kupitia video kwenye mtandao wa Twitter wa klabu yake mpya.

“Nafurahia kuwa sehemu ya familia ya Sagan Tosu. Ningependa kushirikiana na wenzangu kama timu na kufanya vyema. Asante,” alisema Dunga ambaye alichezea klabu za Congo United, SoNy Sugar, Tusker na Nakumatt nchini Kenya kabla ya kuelekea Bara Ulaya mwaka 2016.

Alichezea Acharnaikos nchini Ugiriki kwa miezi mitano kabla ya kuelekea Kusini mwa Afrika kuhudumia City of Lusaka FC na Napsa Stars kwenye Ligi Kuu ya Zambia mnamo Agosti 2017 na January 2018.

Msimu huu wa 2020-2021, Dunga alifungia Vllaznia mabao manne katika michuano saba iliyopita na goli moja kwenye Kombe la Albania (Kupa E Shqiperise).

Mashabiki wa J1 League watatumai wamepata shujaa mwingine kutoka Kenya kama Olunga aliyetetemesha kwenye Ligi ya Daraja ya Pili Japan mwaka 2019 akifunga mabao 27 na Ligi Kuu mwaka 2020 alipopachika goli moja zaidi akiibuka Mchezaji Bora wa Mwaka na pia kutwaa Kiatu cha Dhahabu anachopewa mfungaji bora. Olunga alikuwa na Kashiwa Reysol kwa misimu miwili na nusu kabla ya kuhamia mabingwa wa Qatar, Al Duhail mnamo Januari 12, 2021.

Dunga alikuwa amejiunga na Vllaznia mnamo Agosti 31, 2020 kwa kandarasi iliyotarajiwa kukatika Juni 30, 2021. Tovuti maarufu ya masuala ya soka Transfermarkt, imeweka thamani ya juu ambayo Dunga amewahi kuwa nayo sokoni kuwa Sh16,718,619 mwezi Januari 2020. Pia, ndiyo imefichua urefu wa kandarasi ya Dunga katika klabu ya Sagan Tosu.

Ligi Kuu ya J1 ya mwaka 2021 itang’oa nanga Februari 26, siku mbili baada ya Dunga kusherehekea kugonga umri wa miaka 28.

Mechi ya kwanza ya Sagan itakuwa dhidi ya Shonan Bellmare mnamo Februari 27.

You can share this post!

BBI: Kizaazaa Raila akizuru Githurai

BI TAIFA JANUARI 27, 2021