• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Jepchirchir aahidi kuwika katika mbio za Italia

Jepchirchir aahidi kuwika katika mbio za Italia

Na CHRIS ADUNGO

MWANARIADHA Joshua Cheptegei wa Uganda ‘amemtumia salamu’ Mkenya Kibiwott Kandie ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 21.

Cheptegei ametangaza kwamba atakuwa akiwania nishani mbili za dhahabu katika mbio za kilomita 5,000 na kilomita 10,000 kwenye Olimpiki za Tokyo, Japan mnamo 2021.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alivunje rekodi za dunia kwenye fani hizo mbili mwaka huu. Alisajili muda wa dakika 26:11 kwenye mbio za 10,000 mnamo Oktoba jijini Valencia na kuivunja rekodi ya dakika 26:17.53 iliyowekwa na Mwethiopia Kenenisa Bekele mnamo 2005.

Miezi miwili kabla ya ufanisi huo, Cheptegei alikuwa amevunja pia rekodi ya miaka 16 ya dakika 12:37 iliyowekwa na Bekele kwenye mbio za mita 5,000 kwa kusajili muda wa dakika 12:35.36 kwenye Monaco Diamond League nchini Ufaransa.

Iwapo Cheptegei ambaye huvalia viatu aina ya Dragonfly kutoka kampuni ya Nike atatwaa medali za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 jijini Tokyo mwakani, basi atakuwa mwanariadha wa nane kwa upande wa wanaume kuwahi kufikia rekodi hiyo kwenye fani hizo mbili.

Mapema wiki hii, Kandie alisema anapania sasa kutwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki zijazo za Tokyo japo hajawahi kushiriki mbio hizo ambazo zimekuwa zikitamalakiwa na Bekele pamoja na Mwingereza Mo Farah katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

“Sijawahi kushiriki mashindano ya mita 10,000 lakini nahisi kwamba nina uwezo wa kushinda medali ya dhahabu katika fani hiyo ndiposa nimeamua kuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Kenya katika mbio hizo jijini Tokyo mwaka ujao,” akasema.

Kwa mujibu wa kalenda mpya ya msimu wa 2021 iliyotolewa na mkurugenzi wa michezo katika Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Paul Mutwii mwezi jana, uteuzi wa kikosi kitakachopeperusha bendera ya Kenya nchini Japan katika mbio za mita 10,000 utafanywa Juni 26-27, 2021 jijini Nairobi.

“Kushiriki mbio hizi kutachangia kuimarika kwa kasi yangu kadri ninavyolenga kuvunja rekodi yangu ya nusu marathon kwa kusajili muda wa dakika 56:00 mnamo 2021. Hili ni jambo ambalo nimekuwa nikilijaribu mazoezini na ninaamini linawezekana,” akaongeza Kandie aliyetumia Valencia Half Marathon kuvunja rekodi ya dunia ya nusu marathon (58:01) iliyowekwa na Mkenya Geoffrey Kamworor mnamo 2019 jijini Copenhagen.

“Tangu mwaka wa 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala mbio hizo mita 10,000 katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu katika fani hiyo. Tunalenga kutafuta suluhu katika mbio za mita 10,000 na mita 5,000 ambazo Kenya haijashinda kwa upande wa wanaume kwa muda mrefu,” akasema Mutwii.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutia kapuni nishani ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za Seoul, Korea Kusini mnamo 1988.

Wakati uo huo, Dorcas Tuitoek Jepchirchir anapigiwa upatu wa kutamalaki mbio kilomita 10 za BOclassic zitakazoandaliwa Disemba 31, 2020 mjini Bolzano, Italia.

Mbio hizo ambazo zimepagazwa jina New Year’s Run zinatarajiwa kumpa Jepchirchir jukwaa mwafaka zaidi la kujinyanyua na kuwa miongoni mwa washindi watatu wa kwanza baada ya kukosa pia nishani katika Nusu Marathon ya Dunia iliyoandaliwa jijini Gdynia, Poland mnamo Oktoba 17.

Atajibwaga ugani wiki chache baada ya kunogesha kivumbi cha Valencia Half Marathon nchini Uhispania.

“Nilianza mazoezi ya kivumbi hiki pindi baada ya kutoka Uhispania. Lengo langu ni kuwa katika orodha ya washindi watakaotuzwa medali. Ufanisi huo utanipa motisha zaidi ya kutawala mashindano ya Mbio za Nyika za Afrika zitakazoandaliwa jijini Lome, Togo mnamo Machi 6, 2021,” akasema bingwa huyo wa zamani wa mbio za kilomita 10 za Paderborn, Ujerumani.

Jepchirchir alishiriki mbio za kilomita 21 kwa mara ya kwanza mnamo 2019 alipoambulia nafasi ya pili kwenye mbio za Istanbul Half Marathon nchini Uturuki. Alisajili muda bora wa binafsi wa dakika 66:33 kwenye kivumbi hicho. Baadaye mwake huo, alikamilisha mbio za Copenhagen Half Marathon nchini Denmark katika nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 66:36.

“Nimekuwa nikifanya vyema katika mbio za nusu marathon na vipute vya kilomita 10. Azma yangu ni kuendeleza rekodi nzuri katika mashindano hayo kwa matumaini ya kurejeshwa kwenye kikosi kitakachokuwa kikiperusha bendera ya Team Kenya kwenye mbio za kilomita 21 mwakani,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Diego Costa sasa kutua Arsenal au Wolves

AK yatoa ratiba kali ya Mbio za Nyika kwa maafisa wa...