• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
AK yatoa ratiba kali ya Mbio za Nyika kwa maafisa wa magereza na KDF

AK yatoa ratiba kali ya Mbio za Nyika kwa maafisa wa magereza na KDF

Na CHRIS ADUNGO

KUKAMILIKA kwa awamu ya tatu ya msururu wa Mbio za Nyika za Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) mnamo Januari 2 katika uwanja wa Ol Kalou People’s Park, Kaunti ya Nyandarua kunatarajiwa kupisha duru za mashindano ya kupokezana vijiti mnamo Januari 9 ugani Nyayo, Nairobi.

Haya ni kwa mujibu wa mabadiliko kwenye kalenda mpya ya matukio ya AK katika kampeni za msimu wa 2020-21.

“Mbio za Ol Kalou zitaandaliwa na tawi la AK Nyandarua kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Nyandarua,” akasema mwenyekiti wa AK katika eneo la Kati ya Kenya, David Miano.

“Tunatarajia idadi kubwa ya wanariadha wazoefu na chipukizi kunogesha mapambano hayo ikizingatiwa kwamba ndiyo duru ya mwisho katika Mbio za Nyika katika kiwango cha kaunti,” akaongeza.

Duru za Mbio za Nyika za kaunti zilifunguliwa katika uwanja wa Machakos People’s Park mnamo Novemba 28 na zikatawaliwa na Hellen Obiri na Daniel Simiu katika kategoria ya wanawake na wanaume mtawalia.

Sheila Chelangat na Charles Yosei walitamalaki duru iliyofuatia katika vitengo vya wanawake na wanaume mtawalia katika eneo la Mosoriot, Kaunti ya Nandi mnamo Disemba 19.

Baada ya kivumbi cha kupokezana vijiti uwanjani Nyayo mnamo Januari 9, Mbio za Nyika za Kenya Police Service zitaandaliwa mnamo Januari 15 uwanjani Ngong Racecourse kabla ya zile za Kenya Prisons Service siku moja baadaye katika eneo la Ruiru.

Kaunti zote zitaandaa mashindano yao ya mbio za nyika mnamo Januari 16 kabla ya Majeshi ya Kenya (KDF) kufanya uteuzi wao mnamo Januari 29 katika eneo la Moi Air Base Eastleigh, Nairobi. Mashindano ya Mbio za Nyika katika kiwango cha kimaeneo yatafanyika Januari 30.

Mbio za Nyika za Kitaifa zimeratibiwa kufanyika Februari 13 katika Kaunti ya Kisii na zitatoa jukwaa mwafaka kwa AK kuteua kikosi kitakachopeperusha bendera ya Kenya kwenye Mbio za Nyika za Afrika zitakazoandaliwa jijini Lome, Togo mnamo Machi 6, 2021.

You can share this post!

Jepchirchir aahidi kuwika katika mbio za Italia

Olunga kulenga juu zaidi baada ya makali yake ugani...