• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Duniani yathibitisha Kenya imepata tiketi mbili zaidi

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Duniani yathibitisha Kenya imepata tiketi mbili zaidi

Na GEOFFREY ANENE

Elizabeth Akinyi na Elly Ajowi ni mabondia wa hivi punde kutoka Kenya kufuzu kushiriki Olimpiki 2020 jijini Tokyo. Kenya sasa ina mabondia wanne.

Jopo la kushughilikia fani ya masumbwi katika Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Duniani (IOC) imetumia Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) baruapepe ikithibitisha kuwa Akinyi na Ajowi wamepata tiketi kutokana na viwango vyao bora vya jopo hilo (BTF).

Akinyi atashiriki kitengo cha kinadada cha uzani wa kutoka kilo 64 hadi kilo 69 naye Ajowi atapigania ubingwa wa uzani wa kati ya kilo 81 na kilo 91).

Wawili hao wote walitwaa medali za shaba katika mashindano ya kufuzu kushiriki Olimpiki ya Bara Afrika jijini Dakar, Senegal mwezi Februari 2020.

Wanaungana na Nick Okoth (uzani wa kati ya kilo 52 na 57) na Christine Ongare (kilo 48-51), ambao walipata tiketi moja kwa moja walipofika fainali katika vitengo vyao jiji Dakar.

Jopo hilo lilifutilia mbali mchujo wa mwisho wa kuingia Olimpiki mwezi uliopita uliofaa kufanyika jijini Paris nchini Ufaransa mwezi Juni kutokana na masharti ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Aidha, mabondia 16 wa timu ya taifa ya Kenya almaarufu Hit Squad wataelekea jijini Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hapo Jumamosi kushiriki mapigano ya Ukanda wa tatu mnamo Machi 20-26.

Itakuwa mara ya kwanza timu hiyo ya kocha Benjamin Musa inashiriki mashindano baada ya karibu mwaka mmoja kutokana na mashindano mengi kusimamishwa kwa sababu ya mkurupuko wa virusi vya corona. Italenga kutumia mashindano hayo kupima utayari wake wa mashindano.

  • Tags

You can share this post!

Mganda Wadri na raia wa Rwanda Mbungo wafagia tuzo bora za...

Amejipata tajiri kwa kuwashonea wateja nguo kwa ustadi mkuu