• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Katambe! Ngoma ya EPL yaanza rasmi leo Ijumaa

Katambe! Ngoma ya EPL yaanza rasmi leo Ijumaa

NA MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

MABINGWA watetezi Manchester City watazamiwa kuendeleza ukatili wao dhidi ya Burnley watakapokutana katika mchuano wa kufungua Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu 2023-2024, ugani Turf Moor leo Ijumaa usiku.

Ni mechi inayotarajiwa kuwa mtihani mkali kwa wenyeji Burnley, wanaorejea kwenye daraja ya kwanza baada ya kushinda ile ya pili, Championship, msimu uliopita.

Burnley, maarufu Clarets, wananolewa na nyota wa zamani wa City, Vincent Kompany.

Vijana wa kocha Pep Guardiola walilima wa Kompany 6-0 kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Uingereza (FA Cup) msimu uliopita.

Mambo huenda hayatakuwa tofauti ikiwa Burnley hawatajituma kwa udi na uvumba.

Clarets wamepoteza mechi 11 mfululizo dhidi ya Man-City kwa jumla ya mabao 40-1.

Mkazi na mwenyeji wa Lamu, Jefwa Kalu, ambaye ni shabiki wa Chelsea, asema Manchester City watatandika Burnley mabao 3-1. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hata hivyo, siku ya kwanza inaweza kuwa na mambo yake. Baada ya kuimarisha kikosi katika kipindi hiki cha uhamisho, Burnley inaweza kutoa ushindani ikitafuta pia mwanzo mwema.

Burnley walipepeta mabingwa watetezi Chelsea 3-2 ugani Stamford Bridge katika mechi ya kufungua msimu 2017-2018, kwa hivyo wanaweza kufanya miujiza dhidi ya Man-City.

Hakuna klabu imewahi kushinda EPL mara nne mfululizo, lakini Man-City inaonekana pazuri kubadili hayo baada ya kufagia mataji matatu — EPL, FA na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uliopita.

Man-City, walio katika orodha ya klabu zinazopigiwa upatu kutwaa taji la msimu huu, wameshinda mechi 11 za kufungua kampeni za misimu 12 iliyopita.

Japo leo Ijumaa watafungua EPL wakiuguza kichapo baada ya kulemewa na Arsenal kwenye taji la ngao – Community Shield – uwanjani Wembley, Uingereza, Jumapili iliyopita.

Kesho Jumamosi itakuwa zamu ya Arsenal kuvaana na Nottingham Forest ugani Emirates, Chelsea na Liverpool ni Jumapili uwanjani Stamford Bridge nao Manchester United wataalika Wolves uwanjani Old Trafford mnamo Jumatatu usiku.

  • Tags

You can share this post!

Raila atafutiwa mfupa

Limbukeni Shanderema walipuliwa na St Anthony’s

T L